NA DIRAMAKINI
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman,Oktoba 30, 2022, amekabidhi kile kilichoitwa “Dhamira ya Mageuzi Tanzania” kwa Uongozi wa Taifa wa chama hicho.
Mheshimiwa Othman ametekeleza hilo huko Magomeni Mikumi kwa Sheikh Yahya jijini Dar es Salaam, wakati wa Shamrashamra za Ufunguzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya ACT-Wazalendo.
Ni kufuatia hatua ya ‘surprise’ yake kwa Uongozi wa Kitaifa wa Chama hicho, pale alipokabidhi Kasha, Mlango na Picha Maalum zinazomuonyesha Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, katika harakati wakati wa uhai wake.
Miongoni mwa picha hizo, lilizopukutisha machozi, furaha na kuwacha vinywa-wazi, baadhi ya watu waliokuwepo hapo, zimeonekana kuwagusa hata Viongozi wa Kimataifa wa Kisiasa, waliokuja kuwakilisha Vyama vyao, katika hafla hiyo.
Baadhi ya Picha hizo, zimemuonyesha Maalim Seif akiwepo katika Muonekano wa ‘Haiba ya Juu’ zama za uhai wake, wakati ambao aliwasili ughaibuni, huko Mataifa ya Magharibi, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuendeleza Mapambano ya Kutafuta Haki, na Kutetea Mageuzi ya Kisiasa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesikika akiitaja hatua hiyo, kama zawadi yake na sehemu ya Sherehe hizo, bali pia kama kwamba ni ‘Ufunguzi wa Matumaini Mapya’ katika safari ya mapambano ya mageuzi ya kweli Tanzania, ambayo ni Dhamira ya Maalim, hadi mwisho wa uhai wake.
Ufunguzi wa Jengo hilo umeongozwa na Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Mhe. Zitto Zuberi Kabwe, sambamba na Viongozi wengine Maalum.
Katika Ufunguzi huo, wamehudhuria pia Viongozi mbali mbali, wakiwemo Wawakilishi wa Taasisi na Vyama vya Siasa, kutoka Ndani na Nje ya Nchi.
Jengo hilo jipya limepewa jina la Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye hadi mwishoni mwa uhai wake, alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo.