ALIKATAA KUNIPELEKA ZANZIBAR

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati fulani nikiwa mkoani Iringa nilikuwa na rafiki yangu mmoja niliyesoma naye, rafiki yangu huyu mzaliwa wa Wawi, Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Ndugu yangu huyu alikuwa rafiki yangu mno, naweza kusema inawezekana damu yangu na yake zilipendana mno kama waswahili wasemavyo tulikuwa watu tulioshibana mno. Nina hakika msomaji wangu na wewe unaye rafiki yako mlioshibana pia.

Tulishirikiana sana katika mambo mbalimbali, langu lake na lake langu. Hapa Iringa tulikuwa tunasoma wote kozi moja, lakini mimi nikimtangulia mwaka mmoja.

Nakumbuka kuna wakati tulikuwa tunafanya uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanachuo na mimi nikigombea nafasi fulani, ndugu yangu huyu aliniunga mkono kwa asilimia 100, hatua kwa hatua hadi tukakamilisha lengo letu na tulishinda japokuwa tulikuwa ni kundi la wagombea makabwela.

Urafiki huu na ndugu yangu huyu uliendelea sana, huku na mimi sasa nikivutiwa kwenda Pemba nikafute kiu changu cha macho.

Kwa kipindi cha miaka miwili hapo chuoni nilibaini kuwa ndugu yangu huyu alikuwa ni mtoto wa kiongozi mmoja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati fulani marehemu Dkt.Omari Ali Juma.

Jina la rafiki yangu huyu anafahamika kama Hafsa Omari, Binti Juma. Akiwa mtoto wa mwisho mwisho kwa Dkt. Omari Ali Juma aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa Serikali ya Rais Benjamin Mkapa. (Awamu ya tatu kipindi cha miaka mitano ya kwanza)

Kwa hakika Hafsa Omari alikuwa rafiki yangu sana, muda wote huo mwanakwetu nilikuwa namsisitiza sana siku zote anipeleke Zanzibar.

“Zanzibar yote ina mikoa mitano; Unguja ina mikoa mitatu Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi. Nayo Pemba ina mikoa miwili; Kusini Pemba na Kaskazini Pemba. Unguja ikiwa na wilaya saba nayo Pemba wilaya nne na jumla kuu za wilaya ni kumi na moja.”

Hafsa Omari aliniambia hayo, binti huyu alikuwa na sifa kubwa tatu kwanza alikuwa akiweza kuzuia hasira yake, pili alikuwa mcheshi sana na tatu alikuwa mwanasiasa makini jukwaani anapoomba kura nafasi yoyote aliyogombea au kumnadi mgombea anayemuunga mkono lazima akubalike kwa wapiga kura.

Hapo chuoni akiwa waziri wetu wa habari. Nakumbuka mwalimu wetu wa siasa alikuwa Kilumbi Ngenda wakati huo akiwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa (sasa ni Mbunge wa Ujiji Kigoma).

Mwanakwetu masomo yaliendelea huku nikiendelea kumkumbusha binti Jumaa safari ya Wawi-Kusini Pemba na raha ya safari ya Zanzibar upelekwe na mwenyeji siyo kujiendeaendea tu.

Nakumbuka kuna wakati Iringa Mjini miezi ya sita kunakuwa baridi na upepo mkali, kuna siku nikiwa na ndugu yangu huyu tunaandaa gazeti la Chuo la Tumaini Hill mjadala ulikuwa hali ya baridi hiyo ilivyokuwa. Hafsa Omari alisema kuwa Iringa ilikuwa na baridi inayolingana na ya Lushoto.

Nikamuuliza wewe wa Wawi, Chakechake, Kusini Pembe, Lushoto Tanga ulikwenda kufanya nini? Au ni mbilini kwako? Akanijibu kuwa yeye kuolewa bado, bali kule alikuwa masomoni Shule ya Sekondari Kongei tangu kidato cha kwanza hadi ya cha nne.

Tukiwa hapo alitusimulia habari nyingi za Mji wa Lushoto, huku na mimi nikimtania kuwa akiolewa itapendeza sana kama Msambaa wa Lushoto amuoe maana huko ameshakaa, yeye akicheka tu.

Kutokana na kuwa jirani na Hafsa nilitamani mno kuifahamu shule hii aliyosoma kwa kuwa tabia za Hafsa zilikuwa njema na za kuvutia. Akilini mwangu nikaweka ahadi kuwa binti zangu lazima watasoma shule hii aliyosoma rafiki yangu huyu.

Kweli nililonuia 2006 nililikamilisha Oktoba 15, 2022 kwani nilihudhuria mahafali ya binti yangu Evon Makwega aliyehitimu kidato cha nne Shuleni ya Sekondari Kongei yenye kidato cha kwanza hadi cha sita.

Mahafali haya yalifanyika vizuri huku ikitolewa ahadi kuwa kwa wanafunzi wote 21 wanaohitimu kidato cha nne walikaribishwa warudi kusoma hapo hapo kidato cha tano na sita kwa kupunguziwa ada kwa shilingi 500,000 kila mmoja. Shule hii inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga ni ya wasichana pekee na huku ufaulu wake ni mzuri.

Nikiwa katika mahafali haya nikamkumbuka Hafsa Omar Juma ambaye ndiyo chanzo cha mimi kuifahamu shule hii na nilikumbuka pia namna ndoto yangu ya kupelekwa Zanzibar na mwenyeji haikukamilika hadi kesho.

Kama nilitamani kupeleka binti yangu shule hii ilikamilika nina hakika nitamtafuta tena Hafsa Omar Binti Juma anipeleke Zanzibar nikayashuhudie yale yote aliyonisimulia.

Raha ya safari ya Zanzibar Mwanakwetu upelekwe na mwenyeji ama atakataa kunipeleka Zanzibar?

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news