BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 47

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...mara nyingi wanawake huwa na huruma kwa watoto wao wa kuzaa, lakini ilikuwa tofauti kabisa kwa mama yangu mzazi. Yeye alitokea kunichukia toka nilivyomuokoa Ndolimana mikono mwa wachawi.

Endelea...

Tukiwa kwenye shughuli yetu ya kumwaga dawa kambini hapo, tulimshuhudia BUNDI WA GAMBOSHI akitua kwa mbwembwe kambini hapo.

THE BOMBOM nikatabasamu kwa kujua shughuli tulikuwa tumeimaliza, mbali ya usafiri wa kwenda Heaven na maeneo mengine.

BUNDI WA GAMBOSHI alitumika pia kwenye vita, rejea vita iliyochukua maisha ya viongozi wetu wakuu wa kambi. Ni huyu bundi ndiye aliyeniokoa mikononi mwa Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Tuliendelea kumwaga dawa kambi nzima huku tukipishana na misukule na wachawi wengine kambini hapo.

Baada ya kumaliza kumwaga dawa zetu, tuliondoka eneo hilo tukaenda kusimama mbali kidogo. Tukachukua dawa ya mgorogojo tukaichanganya na dawa ya mjele akatokea panzi mkubwa.

Yule panzi tulimchanganya na madawa mengine kisha tukamuagiza jambo. Punde si punde panzi huyo aliruka na kueleke kwenye kambi ile, baada ya sekunde kadhaa alitua kwenye kambi hiyo.

Ghafla moto wa kutisha ulizuka kwenye jengo moja la kambi hiyo, ulikuwa ni moto mkubwa usio na mfano.

Tukawashuhudia Padri Jonasi na kundi lake wakitoka kwenye jengo la mkutano. Walipofika eneo hilo walianza kumwaga madawa ya kuzima moto huo lakini hawakufanikiwa.

Moto uliwaka! Ukawaka! Ukawaka mpaka jengo lote likateketea. Baadhi ya misukule waliokuwa ndani ya jengo hilo, waliungua na kuteketea kabisa. Thamani zote zilizokuwa ndani ya jengo hilo ziliteketea, yote haya yalifanyika mbele ya macho yetu.

Yule panzi alipaa na kutua kwenye jengo jingine likawaka moto, Padri Jonasi Chambilacho Muzungu na kundi lake walikwenda kuzima moto huo.

Yule panzi alikwenda kutua kwenye majengo mengine mawili nayo yakawaka moto. Hili lilimchanganya kwa kiasi kikubwa Padri huyo na kundi lake.

Katika historia ya kambi hiyo halijawahi kutokea tukio la namna hii. Wakabaki njia panda wakiwa hawana namna ya kufanya.

Wakati huo tulikuwa tumesimama tukishuhudia kila jambo lililokuwa likiendelea kambini hapo. Tulimuona Padri Jonasi na kundi lake wakitapatapa mithili ya mfa maji.

Kwa kuwa hatukuwa tumechoma dawa za kuwazuia misukule kutoroka, walianza kukimbia kila mmoja akitaka kuokoa maisha yake.

Kwa muda huo mfupi walipita misukule zaidi ya mia mbili, wapo waliokuwa wakielekea mji wa Musoma na wengine walielekea mji wa Malagarasi. Kila mmoja alikimbia kunusuru uhai wake.

Kambi hiyo iliendelea kuteketea jengo moja baada ya jingine, hii iliwatia hasira sana Padri Jonasi na kundi lake.

Hata hivyo hawakuwa na uhakika hasimu yao alikuwa nani, yote hii kwa kuwa tulikuwa mbali na eneo hilo.

Japokuwa hawakuwa na uhakika juu ya adui yao, naamini kuwa lazima walikuwa na hisia juu ya kambi yetu. Maana hata jana walikuja kutuchokoza kwenye kambi yetu ya GAMBOSHI MPYA.

Tulipochoma majengo kumi na mbili nilimzuia panzi huyo kuendelea, angalau hali ya hewa katika kambi hiyo ikatulia.

Baada ya hapo tulikwenda kambini hapo tukiwa hatuonekani machoni mwa hasimu wetu. Tulimkuta Padri na watu wake wakijadili juu ya tukio hilo, kila mmoja alikuwa kachukizwa.

Kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kutuona wala kutuhisi, walionekana kuzungumza kwa hasira juu ya tukio hilo.

Padri Jonasi alisikika akisema, "Huyu aliyefanya mambo ya kijinga ni THE BOMBOM. Haki ya Mungu nikimtia mikononi mwangu nitammwaga utumbo wake, hawezi kutuyumbisha hivyo watu wazima. Nitamuua kwa mikono yangu kisha nitamchuna kwa kucha zangu kenge huyo."

Kwa kuwa hakuwa akituona hii ilidhihirisha ni kwa kiasi gani tulikuwa tumemzidi nguvu za madawa. "Hahaaaaaaa! Hahaaaaaaa! Hahahahahahaaaaaa!" Ilisikika sauti ya vicheko kutoka kwetu, Padri na washirika wake wakapigwa na butwaa.

Ghafla tukajitokeza machoni mwao, wakawa wanatuona kawaida kama ilivyo ada japo katikati yetu kulikuwa na umbali mkubwa tuliotengwa na madawa.

Hawakuwa na namna yeyote ya kutufanya kwa kuwa tayari zindiko lako la kambi tulikuwa tumelizindua.

Nilisogelea Padri huyo nikamnasa kibao, kabla ya kudondoka chini nilimuongezea kelebu iliyomdondosha chini. Wale wasaidizi wake walikuwa wamepigwa butwaa huku wakiwa hawajui la kufanya.

Yote haya yalikuwa ni kazi ya nguvu za madawa tuliyomwaga kambini hapo. Nilimnyanyua nikamtwisha kichwa cha mdomoni, akatema meno mawili harafu akajibwaga chini mithili ya gunia la mahindi.

Kisha nikamfuata baba yangu mzazi, nikamkanyaga teke la tumbo akainama kwa maumivu makali. Akiwa bado kainama nilimfyeka mtama akapaa juu mithili ya njiwa kisha akatua kwa makalio.

Mara alianza kulia "THE BOMBOM mwanangu nisamehe baba kwa uovu niliokufanyia, nilidanganywa na Padri Jonasi na Amri Othman Ally.

"Sikusikiliza ujinga huo, nilichukua tofali lililokuwa karibu na eneo hilo nikalishusha tumboni mwa baba yangu mzazi. Matapishi mazito yaliyochanganyika na damu yalimtoka mdomoni.

Nikamshindilia ngumi za usoni mpaka uso ukabadilika rangi, damu si damu! Nyama si nyama! Alikuwa hatamaniki, nikahakikisha nimemuua kwa mikono yangu baba yangu mzazi. Baada ya kukamilisha hatua hiyo, angalau moyo wangu ulitulia kwa kulipa kisasi kwa mzazi wangu mmoja.

Nikawaruhusu wasaidizi wangu kuwashughulikia wachawi wote wa kambi hiyo, ilikuwa ni siku ya furaha kwa upande wangu.

Tuliwafanyia kitu mbaya mbele ya viongozi wao, baada ya hapo tulilipua kambi nzima na kuwaacha wakiteketea kwa moto. Hakuna kitu kilichobaki katika kambi hiyo, vyote viliungua na kuteketea kabisa.

Ndugu msomaji kuna baadhi ya dawa za kichawi huwa haziungui moto, mara nyingi dawa zenye gharama kubwa huwa zinachanganywa dawa zingine za kuzilinda.

Mfano dawa hizo zikichanganywa na maji kwa bahati mbaya huwa haziloi, hata kama zitachomwa moto huwa zinaruka motoni na kukaa eneo salama.

Yote hii huwa zimechanganywa na dawa zingine, Kwa kuwa tulilijua hilo ndiyo maana tulimwaga dawa kambi nzima ya kupoza dawa zote za kambi hiyo.

Tulipolipua kambi hiyo hakuna kilichosalia, kambi nzima iliteketea isipokuwa wale misukule walioondoka mapema.

THE BOMBOM nilijawa na furaha angalau kulipa kisasi kwa mzazi wangu pamoja na kwa wakuu wa kambi waliouliwa na Padri Jonasi.

Kwa kuwa hatukuwa na jambo jingine tuliamua kuondoka, wenzangu walipanda nyungo mimi nilichukuliwa na BUNDI GAMBOSHI.

Tuliondoka eneo hilo nikiwa nimemuomba bundi huyo anipeleke nyumbani kwetu pale Mlyabibi, sikutaka kumuacha mama yangu mzazi akiwa hai.

Roho yangu ingefarijika kuona inalipa kisasi hata kwa mama huyo, kukosekana kwake kambini hapo haikuwa tiketi ya kumuacha hai.

Tulishuka Mlyabibi jirani na nyumbani kwetu, kwa kuwa maeneo hayo ndiyo nimezaliwa bado niliyakumbuka ipasavyo.

Nilikwenda hadi nyumbani kwetu, muda huo ilikuwa ni usiku wa manane. Nilipofika nyumbani hapo nilienda kwenye ukuta wa chumba ambacho baba na mama walikuwa wakilala, nikaegemea kisha nikayeyuka na kuingia ndani.

Chumbani humo hakukuwa na mtu yeyote, nikazisogelea kanga zilizokuwa zimetundikwa chumbani nikaivuta moja nikijua ni kanga ya mama.

Wachawi huwa tuna njia nyingi za kujua mtu anayemtaka yuko wapi wakati huo. Niliinusa kanga hiyo nikagundua mama alikuwa njiani akitokea makaburi, kumbe siku hiyo alipewa kazi maalumu na mkuu wao.

Ndiyo maana hakuonekana kule kambini, niliamua kumsubiri hadi atakapokuja ili nimalizane naye. Muda mchache nikiwa chumbani humo nilishuhudia mlango unafunguliwa kwa matako.

Zipo njia nyingi za kuingia ndani zinazotumiwa na wachawi, njia ya kwanza ni kupitia tundu lolote lililopo kwenye nyumba.

Njia ya pili huwa tunatumia kona ya nyumba, pembe ya nyumba huachana hivyo kuruhusu kuingia au kutoka.

Njia nyingine ni kuegemea kwenye ukuta wa nyumba unayotaka kuingia, ndani ya sekunde kadhaa huwa tunayeyuka na kuingia ndani. Njia ya mwisho ndiyo hiyo ya kuingia kwa matako, mara nyingi huwa inatumiwa na wachawi wengi.

Kwa kuwa mama yangu mzazi hakuwa akijua kuwa nimo ndani, aliingia kwa kujiamini. Wakati anaingia nilimuwahi nikamkamata vyema shingo lake, alipigwa na butwaa katika hali hiyo.

Hakutegemea kukutana na hali hiyo, katika purukushani zetu aliweza kunitambua. "THE BOMBOM naomba uniambie tuzungumze mwanangu, nitakueleza mwanzo mwisho kisa cha kukufanya msukule" aliongea huku jicho akiwa kalitoa kama kurunzi la gari ya mzigo.

Nikaendelea kumbana kwa nguvu zote huku pumzi yake ikikata, nilizidisha kumbana kwenywe shingo lake huku nikitumia nguvu zaidi.

Nikiwa kwenye harakati za kumkaba zaidi nilishtuka napigwa mgongoni kwa mpigo, nilivyoangalia vyema alikuwa msukule akinishambulia ili kumnusuru bosi wake ambaye ni mama yangu mzazi.

Ndugu msomaji mambo yanazidi kunoga, unadhani nini kitampata THE BOMBOM? Atafanikiwa kumuua mama yake mzazi au atazidiwa ujanja na yule msukule? Ungana na mimi sehemu inayofuata.

NINSOLE ?

THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news