BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 48

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia..nilishituka nikipigwa mgongoni kwa mapigo mfululizo, nilivyoangalia vizuri nilibaini alikuwa ni msukule. Alifanya shambulio hilo kumuokoa bosi wake ambaye ni mama yangu mzazi.

Endelea

Hasira iliongezeka kupita maelezo, nilimsukuma mama akaenda kujigonga kwenye ukuta chumbani mle.
Nikamgeukia yule msukule nikamkata ndoige moja akatambarajika chini, wakati huo mama alikuwa amejiegemeza kwenye ukuta ili apotee kimiujiza. Nilimuwahi nikamshika mguu wake ili kama atapotea tupotee pamoja.

Kwa kuwa nia yake ilikuwa ni kunikimbia aliniwahi akanipiga teke la punda kifuani kwangu nikahisi uchungu usiyomithilika.

Tayari yule msukule alinirukia mfano wa nyani na kunikalia kifuani, nikapindua miguu kwa juu nikamkaba shingoni mwake kupitia miguu yangu.

Tayari nilikuwa nimebaini kuwa yule msukule ni mlinzi wa mama, kwa kuwa alikuwa na nguvu za ziada maungoni mwake.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji wachawi baadhi huwa na walinzi katika shughuli zao za kichawi. Walinzi hao hupatikana kutoka kwenye jamii, mfano endapo mtaani kuna bwana mkorofi sana na hujishughulisha na shughuli za ukorofi mara kwa mara huyu huwa na sifa za kuwa msukule mlinzi.

Mtu huyu anaweza kuchukuliwa kwa njia mbalimbali, mfano anaweza kuugua kichwa kwa muda mfupi na kufa.

Njia nyingine ni kwa ajali, anaweza kugongwa na gari mkashuhudia ajali hiyo kumbe aliyegongwa ni sokwe, msukule, mbwa au mgomba.

Hii ni sayansi ndefu kuifafanua, lakini tambua kuna hiyo njia. Njia nyingine ni ile ya yeye kupigwa na mwenzake kwa bahati mbaya.

Unaweza kutokea mzozo baina ya muhusika na mtu mwingine, mara nyingi mzozo huo huwa tunauchochea siye wachawi.

Mzozo huwa mkali kiasi kwamba wataanza kutupiana maneno hatimaye mapigano, hapo ndipo anaweza kupigwa sehemu na kudondoka chini hatimaye kufa.

Kumbe ni kiini macho tu mtu huyo amechukuliwa kwa ajili ya kuwa mlinzi uchawini. Watu hawa hufanya kazi nyingi sana wanapokuwa misukule, kwa mfano wao ndiyo hutumiwa kuwashikisha adabu misukule wenye tabia mbaya.

Hawa pia hutumiwa kumlinda mchawi katika hatari fulani maana huwa wameongezewa dawa maungoni mwao. Misukule hawa si wa kawaida, hujazwa dawa za kutosha kwa ajili ya kupambana na wapinzani wa wachawi.

Japo uchungu na maumivu vilisikika mwilini mwangu, lakini niliendelea kujikaza. Wakati huo miguuni nilikuwa nimemkaba vyema msukule huyo, mkono mmoja nilikuwa nimeshika mguu wa kulia wa mama huku nikiwa chini.

Kwa kanuni za kichawi mama asingeweza kupotelea ukutani pale akiwa kwenye hali ile, endapo angefanikiwa kupotea basi tungepotea pamoja watatu kwa kuwa tulikuwa tumeungana.

Yaani mimi nilikuwa nimeshika mguu mama wakati yule msukule alikuwa kanikalia kifuani huku nikiwa nimemniga kwa miguu.

Ghafla mama alijibetua mpaka akaukaribia mkono wangu niliokuwa nimemshika mguu wake, alining'ata kwa meno yake chonge makali mfano wa mwiba wa nyuki nikamuachia.

Bila kupoteza muda aliegemea kwenye ukuta kisha akapotea, miongoni mwa siku nilizoumizwa hapa duniani ilikuwa ni siku hiyo.

Kumbuka mtu huyu alikuwa ni mama yangu mzazi aliyeshirikiana na baba kunifanya msukule kwa faida yake.

Ni huyu huyu aliyewaua dada zangu na kuwafanya misukule pasi na huruma, ni huyu huyu aliyekuwa akinitesa wakati nikiwa msukule kwenye kambi ya kichawi niliyoiunguza pale darajani.

Huyu alikuwa ni adui namba moja katika maisha yangu, kumuacha hai ni kuhatarisha maisha yangu ya kichawi na kambi yangu kwa ujumla.

Japo nilikuwa nimeiteketeza kambi yao, kumuacha mzima ingekuwa ni mwiba shingoni mwangu kwani angeweza kuungana na wachawi wengine wakanisumbua.

Kwa kuwa mama alikuwa kanizidi ujanja na kutoroka, nilipaswa kumshughulikia huyu msukule aliyekuwa amechangia kwa kiasi kikubwa kutoroka kwa mama.

Niliendelea kumbana msukule huyo kwa miguu shingoni mwake kwa nguvu, kumbuka hapa zilikuwa zikitumika dawa na si mguu wa kawaida.

Kadri nilivyokuwa nikimbana aliendelea kulainika mithili ya chapati za mayai ndani ya kikaangio. Nilimbana akawa anatweta mithili ya mbwa wa msasi, kadri nilivyozidi kumbana macho akawa anayatoa pima.

Mara ulimi wake aliutoa nje ukaning'inia kama ule wa fisi nikatambua kuwa mwendo alikuwa ameumaliza. Nilizidisha kumkaba kwa miguu mpaka nilipojihakikishia kuwa alikuwa ameaga dunia kisha nikaachilia shingo lake.

Nilinyanyuka haraka kisha nikaanza kuchunguza chumbani humo, bahati nzuri nilikiona nilichokuwa nikikitafuta.

Kulikuwa na sanduku la nguo za mama lililokuwa chumbani humo, nililifungua kisha nikabahatika kuona nguo zake.

Niliendelea kuchunguza ndani ya sanduku hilo na hatimaye niliziona nguo za mama za ndani. Niliichukua nguo moja nikanyofoa uzi kisha uzi huo nikaufunga kwenye Kaniki yangu halafu nikaegemea ukutani na kupotea.

Nilimuacha msukule huyo akiwa ameaga dunia chumbani humo, bado hasira ilikuwa imenipanda mwilini mwangu.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa mama yangu mzazi kuponyoka kiajabu ajabu mikononi mwangu. Bado nakumbuka aliwahi kuponyoka kwenye mji wa Mpeta leo pia ameponyoka nikimshuhudia kwa macho yangu.

Baada ya kuegemea kwenye ukuta huo nilitokeza nje ya nyumba, kisha nilikwenda kwenye mwembe mkubwa uliopo nyumbani kwetu.

Mwembe huo naukumbuka vyema kwa kazi yake ya ziada, mbali ya kutumiwa kwa kivuli ulitumika pia kuhifadhi misukule.

Ni huu mwembe uliotumika kunihifadhi kwa muda mfupi nikiwa msukule mara baada ya kuuliwa na wazazi wangu.

Kwenye huo mwembe kulikuwa na misukule wengi, waliponiona tu walikurupuka kila mmoja akawa ananusurisha uhai wake.

Waliruka toka mtini mpaka chini wakawa wanakimbia kuelekea maeneo waliyoona yangekuwa salama maishani mwao.

Wapo walioelekea eneo la makanisani wengine walielekea sehemu zingine.Nilidhamilia kuwachoma moto misukule hao, bahati mbaya waligundua hilo wakatoroka.

Hata hilo kwa upande wangu lilitosha kabisa kuwaaibisha wachawi wa mji wa Mlyabibi. Nilijua kabisa kesho yake kungekuwa na misukule wa kutosha mitaani.

Kwa namna moja au nyingine hili lingewafanya wanakijiji wa mji wa Mlyabibi kuujua ukweli juu ya uchawi.

Niliamini baadhi wangewatambua ndugu zao waliofanywa misukule, na wengine wasingetambulika kwa kuwa ni kawaida ya wachawi kubadilishana misukule. Yawezakuwa walibadilishwa toka nchi za jirani au mikoa na wilaya za mbali zaidi toka hapa Mlyabibi.

Niliachana na misukule hao nikaelekea alipokuwa BUNDI WA GAMBOSHI, nilimkuta akiwa katulia kisha nikaingia kwenye uvungu wa vidole vya miguuni mwake.

Punde si punde aliruka hewani kisha akapiga mbawa zake kwa mbwembwe. Tukaianza safari ya kuelekea kwenye kambi yetu ya kichawi pale majengo karibu na kiwanja cha ndege.

Japo mama mzazi aliponyoka kuuawa mikononi mwangu, bado nilikuwa nikifurahia ushindi mkubwa nilioupata wa kumuua Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Ushindi wa kuchoma na kusambaratisha kambi hiyo ulinipa nguvu zaidi wa kuendelea na ujenzi wa GAMBOSHI MPYA. Mawazo yote hayo yaliniijia kichwani mwangu wakati nikiwa ndani ya uvungu wa vidole vya bundi huyo tukiwa hewani tukielekea kambini kwetu.

Ndugu msomaji endelea kufuatilia sehemu inayofuata, je, THE BOMBOM atatua salama kambini kwake?

WALAYEE?

THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news