Dkt.Kikwete mgeni rasmi ufunguzi Wiki ya Maonesho ya Kimataifa ya Uwekezaji na Biashara mkoani Pwani

NA ROTARY HAULE

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Wiki ya Maonesho ya Kimataifa ya Uwekezaji na Biashara yatakayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Mailimoja Kibaha Mjini.
Wiki ya Uwekezaji na Biashara itaanza kesho Oktoba 5, 2022 na kumalizika Oktoba 10, 2022 ambapo wadau mbalimbali watashiriki ikiwa sehemu ya kuonesha bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vilivyopo mkoani Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge,ametoa taarifa hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo ikiwa sehemu ya kuhamasisha wawekezaji,Wafanyabiashara,wadau na wananchi kushiriki maonesho hayo.

Kunenge amesema kuwa, maandalizi ya shughuli nzima mpaka sasa yamekamilika kwa asilimia 95 na kwamba bado wadau wanakaribishwa kushiriki kwakuwa fursa ipo wazi kwa ajili yao na kwamba mpaka sasa tayari wawekezaji 200 wamethibitisha kushiriki.
"Wiki ya maonesho ya Uwekezaji na Biashara yataanza kesho Oktoba 5 lakini ufunguzi rasmi utafanyika Oktoba 6 na mgeni wetu rasmi ni Rais Mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete,"amesema Kunenge

Aidha, Kunenge ,amesema kuwa katika wiki hiyo yapo mambo mbalimbali yatafanyika ikiwemo Kongamano kubwa la wawekezaji litakalofanyika Oktoba 10 katika Chuo Cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

Amesema, Kongamano hilo litahudhuriwa na wawekezaji mbalimbali ,wataalamu wa kiuchumi, viongozi wa Serikali na taasisi wezeshi huku akiwaomba wananchi wajitokeze kushiriki kongamano hilo ili wapate fursa ya kujua maeneo ya uwekezaji yaliyopo katika Mkoa .
Amesema,lengo kubwa la maonesho hayo ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifanyakazi kubwa kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya wawekezaji.

Kunenge, ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo wananchi watapata fursa ya kujionea bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Mkoa wa Pwani,kupata fursa mpya za uwekezaji, wazalishaji kupata masoko ya uhakika,kujua teknolojia za kisasa.

"Pamoja na faida kuwa nyingi katika maonesho haya ,lakini pia itakuwa fursa kubwa ya kuona jinsi gani sera nzuri na jitihada za Rais zinavyoweza kutoa majibu juu ya masuala ya uwekezaji hapa nchini,"amesema Kunenge

Ameongeza kuwa, maonesho hayo yataonyesha namna ambavyo wawekezaji wa Mkoa wa Pwani walivyopiga hatua ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya nchi katika uwekezaji.
Amesema, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na kwamba amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutumia fursa hiyo kufanya biashara ili wajiongezee kipato.

Hata hivyo, Kunenge amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maonesho hayo ili kuona kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news