NA STEVEN NYAMITI
IMEELEZWA kuwa, Kampuni ya Uchimbaji dhahabu ya Geita Gold Mining Limited (GGML) inaongoza kwa kuwa kampuni ya uchimbaji madini nchini inayofanya vizuri katika kutimiza Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (CSR).

"Mimi ningependa tuwe wa kweli, nchi hii kampuni inayofanya vizuri kwenye CSR kwenye madini ya kwanza ni GGM. Wamefanya kazi nzuri," amesisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, ameipongeza GGM kwa kujenga mahusiano mazuri ya kijamii na wananchi wanaozunguka mgodi huo. Dkt. Biteko amepongeza GGM kwa kuweka mitambo mipya ya kuchenjua mabaki ya kaboni ili kupata dhahabu badala ya kusafirisha kaboni kwenda nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo kabla.

"Tunafurahi kuona kwamba mgodi wa GGM wamejitaidi kuendelea kuweka uzalishaji kuwa kwenye kiwango kinachotakiwa. Kwa mujibu wa taarifa za mgodi, mgodi huo unazalisha Wakia 480,000 hadi sasa, tunawapongeza sana," amesema.

Naye, Makamu wa Rais wa Kampuni ya GGM, Simon Shayo akizungumzia kuhusu utekelezaji wa CSR kwa jamii amesema, kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri katika mazingira yote yanayozunguka mgodi.
Pia, amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuipongeza GGM kwa namna kampuni hiyo inavyojitaidi kwenye kununua bidhaa na kutumia huduma za kitanzania.
"Asilimia kubwa ya bidhaa zetu sasa karibu asilimia 70 ya fedha inayotumiwa na GGM inanunua bidhaa kutoka Tanzania," amesisitiza.

