'Hauwezi kujutia kuwekeza Mara, Kigoma na Kagera fursa ni nyingi mno'

NA DIRAMAKINI

LEO Oktoba Mosi, 2022 viongozi wa mikoa ya Mara,Kigoma na Kagera wameainisha fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo zinapatikana katika mikoa hiyo.
Wameyabainisha hayo kupitia Mkutano wa Zoom uliorushwa na vyombo mbalimbali vya habari chini ya uratibu wa Watcha Tanzania ambapo licha ya kuainisha fursa pia wameelezea namna ambavyo Serikali Kuu imekuwa ikielekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Viongozi hao wamesema kuwa;

MHE. CGF (RTD) THOBIAS E.M. ANDENGENYE, MKUU WA MKOA WA KIGOMA

" Tumepokea shilingi bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 358 kwa mahitaji ya wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza mwakani, hivyo kupunguza wimbi la upungufu wa madarasa katika kipindi hiki cha sera ya elimu bure.
"Mkoa wa Kigoma sasa hivi umeunganishwa na Gridi ya Taifa hii ni wiki ya tatu sasa tumeunganishwa kwa njia ya umeme kutoka Nyakanazi kwenda Kibondo hadi Kasulu, hivyo genereta zilizokuwa zinafanya kazi katika wilaya hizo kuzimwa.
"Mkoa wa Kigoma hapo zamani ulikuwa na changamoto kubwa sana ya barabara, lakini sasa hivi tunamshukuru sana Rais wetu Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wake wa ujenzi wa barabara kuu, hivyo kutufanya kuungana kirahisi nchi jirani zetu kama Burundi, Congo na Rwanda ambapo watu wake huja Kigoma kwa ajili ya shughuli za kibiashara,"amesema.

MHE.ALBERT CHALAMILA, MKUU WA MKOA WA KAGERA

"Kwa upande wa Mkoa wa Kagera suala la uhalifu limepungua kwa kiasi kikubwa sana, kwani Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ajira za kutosha ilikukabiliana na masuala ya ujangili, hivi karibuni tumepokea vijana wa Jeshi la Polisi, Zimamoto, Uhamiaji na majeshi mengine kwa ajili ya kuimarisha usalama wa Mkoa wa Kagera.
"Kagera ni mkoa wa kwanza katika uzalishaji wa kahawa aina ya Arabica na Robusta, kahawa hizi ni hitaji kubwa sana duniani kutokana na ubora wake kwa afya za binadamu, hivyo niwaombe wawekezaji kuja Kagera kufanya utafiti wa kutosha wa zao hili na kufanya uwekezaji katika zao la kahawa ninawaahidi hawatojuta.
"Mkoa wa Kagera una fursa kubwa sana katika kilimo, kwani ni maarufu sana kwa mazao kama ndizi, kahawa,kunde,mahindi n.k, hapo zamani wakazi wa Kagera walitumia ardhi kwa ajili ya kilimo cha kula tu ila hivi sasa wamehamasika kufanya kilimo cha biashara tena cha kisasa na kuongeza kipato chao kupitia mazao hayo,"amesema.

MHE.MEJA JENERALI SULEIMAN MZEE, MKUU WA MKOA WA MARA

"Ziwa Victoria lina fursa nyingi sana za uvuvi, tumeshaanza kuwashawishi watu kuwekeza katika uvuvi wa kutumia vizimba, tunashukuru Jeshi la Wananchi limeshaanza kufanya uwekezaji huo na ni sehemu nzuri sana watu kwenda kujifunza.
"Tarime ni moja ya wilaya zenye rutuba nzuri sana, kule tumeanzisha kilimo cha kahawa hivyo tumekusudia mwaka 2025 tufikishe tani 25,000 kwani hazilimwi kupitia kemikali au organic.

"Mkoa wa Mara una visiwa zaidi ya 37 katika Ziwa Victoria na vyote vimekaa kiutalii na kuvutia, hivyo niwaombe wawekezaji kuja kuwekeza katika visiwa hivyo ni fursa kubwa sana,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news