HEBU ACHA MBIO HIZO-1:Mwatumaliza jamani!

NA LWAGA MWAMBANDE

KAMA wewe ni dereva uendeshaye magari, au wewe kiongozi, uendeshwaye. Ni sheria bila shuruti ndiyo inakutawala?

Au unafanya upendavyo, yaani uko juu ya sheria? Mshairi wa Kizazi kipya, Lwaga Mwambande, kwa njia ya ushairi anafikiri kwamba sheria za usalama barabarani, kwa sehemu kubwa zinafwatilia watu binafsi na vyombo vyao vya moto. Mengine jielimishe na uchukue hatua;

1:Dereva wa daladala, ni bora kuliko wao,
Wasafiri wanalala, walakini siyo wao,
Unashindwa hata kula, sababu ya mwendo wao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

2:Daladala ngalangala, si kama magari yao,
Yanunuliwa kwa dola, lakini hizo si zao,
Kwaendesha na kulala, kupata riziki yao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

3:Zidisha mwendo ni jela, walakini siyo wao,
Kwao ukifunga tela, adhabu yako si yao,
Kuendesha kama kula, ndiyo starehe yao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

4:Usalama wanalala, zisije zikawa zao,
Kwamba wawashike kola, kumbe yumo bosi wao,
Washikwe wapige sala, kupata punguzo lao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

5:Dereva wa daladala, hawaui hovyo hao,
Kariakoo-Mbagala, polepole kasi yao,
Wana njaa wanakula, sehemu ya kazi yao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

6:Pengine si madereva, wa hayo magari yao,
Ambao ndio waiva, kwa kasi ya mwendo wao,
Pengine ni hao nguva, wawapelekesha wao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

7:Nakumbuka bosi yupo, walifanya kazi yao,
Kusema hapo ulipo, mwendo kinyume na wao,
Alofanya cheo kipo, sasa wako wapi hao?
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

8:Kumbukumbu nyingi zipo, vifo vya kwetu na wao,
Huko viongozi wapo, kufa ni mbio zao,
Walioumia wapo, heri salimika yao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

9:Usalama nanyi vipi, jinsi mwaacha hao?
Alosema bosi vipi, twaona wapeta hao?
Hadi wakufe wangapi, ya kwamba wakabwe hao?
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

10:Mabasi weka ribiti, ila si magari yao,
Binafsi wadhibiti, siyo madereva wao,
Hizo ambulensi ati, ukiona mbio zao,
Hebu acha mbio hizo, mwatumaliza jamani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news