NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Afya imetoa ufafanuzi wa maswali yanayoulizwa mara kwa mara na wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nchini.
Baadhi ya wananchi wakipata huduma kwenye Banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika Maonesho ya Kilimo Kitaifa 2022 Nane Nane yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. (Mpigapicha Wetu).
Ufafanuzi huo ambao umetolewa kupitia Toleo la Kwanza Oktoba 9, 2022 umelenga kuwapa wananchi uelewa mpana na kuweza kupata majibu ya maswali ambayo wamekuwa wakijiuliza mara kwa mara kuhusu Bima ya Afya kwa Wote.
Hapa chini ni orodha ya maswali na majibu kuhusu Mapendekezo ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kama yalivyoulizwa na kutolewa ufafanuzi na Serikali kupitia Wizara ya Afya, endelea;
1. Swali:
Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote unaanza lini?
Jibu:
Sheria ya Bima ya Afya kwa wote inatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa na Bunge Novemba 2022. Utekelezaji wake rasimu unatarajiwa kuanza rasmi Julai Mosi, 2023 baada ya kuridhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe Samia Suluhu Hassan.
2. Swali:
Je kutakuwa na NHIF pekee yake au kutakuwa na mifuko mingine?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, mfumo wa bima ya afya nchini utajumuisha bima ya afya ya Umma na Binafsi.
Sheria inayopendekezwa itaitambua NHIF kama Mfuko wa Bima ya Afya wa Umma ambayo itahudumia Watumishi wa Umma na wananchi wengine watakaochagua kujiunga na mfuko huo.
Aidha, Sheria pia inaruhusu kuwepo kwa Skimu binafsi za Bima ya Afya ambazo zitatoa huduma za Bima ya Afya kwa wananchi katika sekta rasmi binafsi na isiyo rasmi.
3. Swali:
Je uchangiaji utakuwa ni kiwango gani kwa mwananchi mmoja mmoja na familia ambao siyo waaajiriwa rasmi?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya kupitia Kanuni ataweka viwango vya uchangiaji kwa kuzingatia uhitaji wa huduma, gharama halisi za matibabu na uwezo wa wananchi kuchangia na mapendekezo yaliyopo yatategemea maoni ya wananchi na ridhaa ya mamlaka zingine.
4. Swali:
Je kwa wananchi ambao ni kaya masikini watahudumiwa kwa utaratibu gani?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, watu wasio na uwezo watakuwa na haki ya kupata huduma za matibabu kupitia utaratibu uliowekwa na Serikali baada ya kuwatambua kupitia mfumo wa utambuzi wa watu wasio na uwezo wa Serikali.
5. Swali:
Je Mwanachama atapata huduma za matibabu sehemu yoyote nje ya mkoa anaoishi?
Jibu:
Mwananchi atakayejiunga na Bima ya Afya atakuwa na fursa ya kupata huduma za matibabu katika vituo vya huduma vilivyosajiliwa na Mfuko katika Mkoa wowote.
6. Swali:
Je kutakuwa na ukomo wa idadi ya wategemezi katika Kaya?
Jibu:
Ndio, Sheria inayopendekezwa itaweka ukomo wa utegemezi ambapo mwanachama anaweza kusajili mwenza na wategemezi wasiozidi wanne kama wanufaika.
7. Swali:
Je huduma za magonjwa yote zitatolewa kwenye Mfumo wa Bima ya Afya kwa wote?
Jibu:
Kitita cha mafao kitakachotolewa kwa wananchi kitazingatia huduma zote zilizopo katika mwongozo wa tiba (STG), Orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu (NEMLIT) na aina ya magonjwa kama ilivyoainishwa katika Miongozo ya Tiba ya Kimataifa (ICD 12). Aidha wananchi watapata huduma hizo kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Taifa.
8. Swali:
Je mwanachama ana haki ya kuhama kutoka Mfuko mmoja kwenda mwingine bila masharti yoyote?
Jibu:
Sheria inayopendekezwa, itaweka fursa kwa baadhi ya makundi ya wananchi kuchagua kujiunga na skimu za bima ya afya kulingana na matakwa yao kwa kuzingatia miongozo itakayowekwa na skimu za bima ya afya zitakazokuwepo.
9. Swali:
Je wananchi wasio kwenye mfumo wa ajira rasmi watatumia utaratibu gani kuchangia?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, wananchi wasio kwenye mfumo wa ajira wana fursa kujiunga na skimu za bima ya afya kama makundi mengine ya wananchi.
10. Swali:
Je kutakuwa na Mamlaka ya kusimamia Mifuko hii ili itoe huduma bora?
Jibu:
Ndio, Skimu zote za Bima ya Afya zitasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) ambayo itakuwa na jukumu la kuhakikisha kila skimu inatimiza vigezo na masharti katika utoaji wa huduma bora kwa wanachama wa bima ya afya. Vilevile, wanachama wana wajibu wa kutoa taarifa pale asiporidhika na huduma zitolewazo.
11. Swali:
Je mwanachama ataruhusiwa kwenda kituo cha ngazi yoyote atakapohitaji kupata huduma za matibabu?
Jibu:
Ili kuhakikisha uhai na uendelevu wa Mfuko, wakati wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, wanufaika wa skimu za bima ya afya watakakiwa kufuata utaratibu wa rufaa wakati wa kupata huduma za matibabu kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Taifa.
12. Swali:
Je Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote imeweka utaratibu gani wa huduma ambazo haziko ndani ya nchi?
Jibu:
Pamoja na ukweli kuwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi ndani ya nchi, Serikali itaendelea kuratibu upatikanaji wa huduma za matibabu nje ya nchi pale itakapolazimika.
13. Swali:
Nini maana ya Bima ya Afya kwa Wote?
Jibu:
Bima ya Afya kwa wote ni mpango unaowezesha wananchi wengi kujumuishwa katika utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua na Serikali kuweka utaratibu kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.
14. Swali:
Nini dhana ya Bima ya Afya kwa Wote?
Jibu:
Bima ya Afya ni utaratibu wa kuchangia kabla kuugua. Dhana ya bima ya afya imejengeka katika msingi wa mshikamano wa kijamii katika kuchangiana gharama za matibabu miongoni mwa wanajamii na hivyo kumudu gharama za matibabu.
Ugonjwa huja bila taarifa, hivyo Bima ya Afya ni uhakika wa matibabu Bima ya Afya inawezesha wenye uwezo na wasio na uwezo wa kipato, wagonjwa na wasio wagonjwa kuchangiana na kupata huduma sawa.
15. Swali:
Kwa nini Serikali imeamua kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote?
Jibu:
Serikali imeamua kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha kundi kubwa la wananchi kuweza kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha na hivyo kuwaepusha kuingia katika janga la umaskini kutokana na gharama kubwa za matibabu.
Hivyo, utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya utawezesha dhamira ya Serikali ya Afya Bora kwa Wote.
16. Swali:
Kuelezea tofauti ya Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Mifuko Mingine.
Jibu:
Tofauti kati aya NHIF na a mifuko ya CHF na Kampuni Binafsi za bima ya afya ukubwa wa wigo wa vituo vilivyosajiliwa vya kutoa huduma nchini, wingi wa huduma zilizo katika kitita cha mafao pamoja na kutokuwepo kwa ukomo wa huduma kwa wanufaika wake.
17. Swali:
Nini faida za Sheria ya Bima ya Afya kama itapitishwa na Bunge?
Jibu:
Baadhi ya faida kubwa za Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ni pamoja
na:-
i) Kuwaepusha wananchi na hatari ya janga la umaskini kutokana
na gharama kubwa za matibabu;
ii) Kuwezesha kundi kuwa la wananchi kupata huduma za matibabu
bila kikwazo cha fedha
iii) Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za matibabu nchini,
iv) Kuwa na mdhibiti na msimamizi wa ubora wa huduma za bima
ya afya nchini na hivyo kuongeza ufanisi wa skimu za bima ya
afya.
18. Swali:
Nini dhana ya kufungamanisha Bima ya Afya na Huduma nyingine?
Jibu:
Ufungamanishaji wa huduma nyingine na bima ya afya una lengo la kuweka msukumo wa wananchi kujiunga na huduma za bima ya Afya kabla ya kuugua.
Bima ya afya itafungamanishwa na huduma za kijamii zifuatazo:-
>Hati ya kusafiria na viza kwa wageni
>Bima za vyombo vya moto
>Utambulisho wa mlipa kodi (TIN)
>Laini za simu
>Uanachama vyama vya ushirika
>Wanafunzi kujiandikisha kidato cha 5 na 6 na vyuo
>Kitambulisho cha uraia (NIDA)
Hata hivyo utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote itakuwa hatua kwa hatua. Hata hivyo, makundi ambayo hayatatakiwa kuingia katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Sheria wataendelea kupata huduma zilizofungamanishwa bila kuhitajika kuwa na Bima ya Afya.
19. Swali:
Je Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote isipopitishwa itakuwa na madhara gani?
Jibu:
Endapo Sheria ya Bima ya Afya haitaridhiwa na Bunge, bado kundi kubwa la wananchi (85%) watakuwa nje ya mfumo wa bima ya afya na kushindwa kumudu gharama za matibabu na hivyo kuwa katika hatari ya kuingia katika umaskini au kifo.
20. Swali:
Je kwenye Sheria hii huduma za Tiba katika vituo vya Umma na Binafsi itakuwaje?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, wananchi wote watakaojiunga na bima ya afya watakuwa na fursa ya kupata huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vikiwemo vituo vya Serikali, Binafsi na vinavyo milikiwa na Madhehebu ya Dini kupitia skimu za bima ya afya watakazojiunga.
21. Swali:
Je sheria ikipitishwa itakuwa na matokeo gani katika huduma za afya mfano upatikanaji wa dawa, huduma za vipimo?
Jibu:
Bima ya Afya ni mpango endelevu na thabiti katika ugharamiaji wa huduma za matibabu kwa kundi kubwa la wananchi.
Hivyo, kupitia utaratibu wa bima ya afya, vituo vitakuwa na mapato ya uhakika na hivyo kuwa na uwezo wa kuboresha huduma za matibabu ikiwemo upatikanaji wa dawa, vipimo, vifaa tiba nk pamoja na rasilimali watu.
22. Swali:
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejiandaaje kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi kwenye vituo vya Umma kama Sheria itapitishwa?
Jibu:
Serikali imeshafanya maandalizi ya kutosha katika mkakati wa Elimu kwa Umma, rasilimali watu, kuongeza miundombinu ya kutolea huduma mijini na vijijini, uimarishaji wa Bohari ya Dawa,kuongeza bajeti ya dawa na kuboresha miongozo ya tiba ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya.
23. Swali:
Changamoto zipi Mfuko wa NHIF na CHF umepitia katika utoaji wa huduma?
Jibu:
Changamoto kubwa ambayo NHIF na CHF imepitia ni ya uhiari wa wananchi kujiunga na Mifuko hiyo hali iliyosababisha wanaojiunga kuwa wagonjwa.
Uhiari umekuwa na madhara kwa Mifuko kutokana na kuhudumia wanachama wachache na wagonjwa ambao wanatumia gharama kubwa kuliko michango ya wanachama husika.
24. Swali:
Nini uzoefu wa Bima ya Afya kwa Wote kwa nchi zingine?
Jibu:
Mchakato wa kuanzisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote umepitia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti na kujifunza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote katika nchi mbalimbali ikiwemo Rwanda na Ghana.
Kwa nchi ya Ghana ambayo inatekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote imefanikiwa kuongeza idadi ya wananchi katika mfumo wa bima ya afya hadi kufikia asilimia 41 ya wananchi wote mwaka 2015.
Kuwepo kwa mfumo madhubuti wa usajili wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya. Kwa upande wa nchi ya Rwanda imefanikiwa kuwepo kwa uwiano (equity) katika upatikanaji wa huduma bora za afya katika ngazi
zote nchini.
Kuongezeka kwa idadi ya wananchi waliojiunga na mfuko kutoka asilimia 7 na kufikia asilimia 90 kwa kipindi cha miaka miwili toka mwaka 2017 hadi Desemba, 2019.
Kuboreshwa kwa huduma za afya kutokana na vituo vya kutolea huduma kuwa na uwezo wa kifedha zinazorejeshwa kutoka Mfuko wa Afya ya Jamii.
25. Swali:
Je Wazee na Wastaafu watapataje huduma chini ya Sheria hii?
Jibu:
Sheria inayopendekezwa, imetoa fursa kwa kila mwanachi ikiwemo wastaafu kuwa na haki ya kupata huduma za matibabu kupitia skimu mbalimbali za bima ya afya zitakazosajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima nchini.
26. Swali:
Je Mfuko wa NHIF kuanzia uanzishwe umeleta matokeo yapi chanya katika huduma za afya?
Jibu:
Tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mwaka 2001, Mfuko umetoa mchango mkubwa maendeleo ya Sekta ya Afya nchini. Mafanikio hayo ni pamoja na:-
i) Kuongeza mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya
ii) Kuwezesha kundi kubwa la wananchi likiwemo watumishi
Umma kupata huduma za matibabu
iii) Kuwezesha wananchi kufahamu dhana na umuhimu wa kuwa
na bima ya afya
iv) Kuweza kutekeleza dhana ya ushirikishaji wa Sekta ya Umma
na Binafsi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi
v) Kutoa uzoefu kwa nchi nyingine kujifunza katika maswala ya
bima ya afya
vi) Kushiriki katika kuboresha miundombinu ya utoaji wa
huduma za matibabu nchini.
27. Swali:
Kutaja Idadi ya Wanufaika na wanachama ndani ya NHIF,CHF na Private hadi kufikia sasa?
Jibu:
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo hadi kufikia mwezi Juni 2022, mfumo wa bima ya afya inajumla ya wanufaika 8,567,486 sawa na asilima 15 ya Watanzania
NHIF- 8%
CHF – 6%
SHIB – 0.01%
Bima Binafsi- 0.09%
28. Swali:
Je waajiri(umma na binafsi) wenye Bima ya Afya na wao watalazimika kuchangia kwa watumishi wao?
Jibu:
Waajiri wataendelea na utaratibu wa awali wa kuchangia asilimia sita ambapo mwajiri anaweza kuchangia asilimia tatu au zaidi na mwajiriwa au mtumishi kuchangia kiasi kilichobaki.
29. Swali:
Serikali imejipangaje kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) ambayo inasemekana yamedhoofisha Mfuko wa NHIF?
Jibu:
Serikali inaendelea na utekelezaji wa program zake za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi ya namna ya kuepukana na magonjwa haya pamoja na uhamasishaji wa wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Kampeni za uelimishaji zinaendelea kuanzia ngazi Taifa na kushuka hadi kwenye mitaa, taasisi, mashule/vyuo na makundi mbalimbali.
30. Swali:
Je Mfuko wa NHIF umejipangaje kudhibiti vitendo vya udanganyifu endapo Sheria itapitishwa?
Jibu:
Mapambano na udhibiti wa vitendo vya udanganyifu ni suala endelevu hivyo Mfuko umeendelea na uimarishaji wa kitengo kinachopambana na udanganyifu pamoja na kuendelea kuwekeza katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA na kutoa adhabu kwa watakaobainika kufanya udanganyifu. Aidha, kitengo cha kudhibiti Fraud kimeimarishwa ndani ya Mfuko.
31. Swali:
Je mwananchi asiyeweza kujiunga na bima ya afya atashtakiwa?
Jibu:
Kupitia Sheria inayopendekezwa, hakuna mwananchi atakayeshitakiwa kwa kushindwa kujiunga na bima ya afya isipokuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wananchi wote kujiunga.
32. Swali:
Kitita cha Mafao cha Msingi kinachopendekezwa kitakuwa na ubora gani kwa wananchi?
Jibu:
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote imeweka haki kwa kila mwananchi atakaye jiunga na skimu yoyote ya bima ya afya kupata huduma zote zilizoainishwa katika Kitita cha mafao cha msingi.
Kitita cha mafao cha Msingi kinachopendekezwa kinalenga kuwezesha wananchi wote kupata huduma kama vile kumwona daktari, huduma za wagonjwa wa nje, kupata vipimo, kupata dawa, kulazwa, upasuaji na huduma za uzazi kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa.
33. Swali:
Je nini maana ya Kitita cha Mafao cha Msingi?
Jibu:
Kitita cha Mafao cha Msingi ni ujumuishaji wa huduma zote muhimu ambazo kila mgonjwa atastahili kulingana na viwango vya michango vilivyowekwa katika Kanuni na kadri Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya atakavyokuwa akiboresha kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam.
34. Swali
Je wananchi wenye bima ya afya binafsi wataendelea kupata huduma za afya baada ya Sheria kupitishwa?
Jibu:
Wananchi wenye bima za afya binafsi kwa mujibu wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote watakuwa na haki ya kuendelea kupata huduma katika bima hizo au kuchagua kujiunga na bima nyingine.
35. Swali
Je mtumishi wa umma anaruhusiwa kuchagua mfuko wowote kujiunga?
Jibu:
Hapana. Mtumishi wa umma ataendelea kupata huduma kwa utaratibu uliopo sasa kupitia skimu ya bima ya afya ya
Umma.
36.
Swali
Je utekelezaji wa sheria hii utakuwa wa mara moja kwa makundi yote baada ya kupitishwa?
Jibu:
Hapana, utekelezaji wa sheria hii utafanywa hatua kwa hatua huku tathmini ikifanywa kila mara kabla ya hatua nyingine kwa kuanzia makundi ya wananchi wenye ajira rasmi (umma na binafsi), wanafunzi wa vyuo, vyama vya ushirika na baadae makundi ya wananchi wasiokuwa na ajira rasmi.
Hatua hizi zina lengo la kuhakikisha wananchi hawakosi huduma zilizofungamanishwa, wanachangia kutokana na
uwezo wao na kufanyika tathmini za kisayansi kabla ya hatua nyingine.
37.
Swali:
Je, wategemezi wanaotwaje katika Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kuwa sehemu ya wanufaika ni kina nani?
Jibu:
Wategemezi watakaojumuishwa na mwanachama kama wanufaika ni wafuatao:
(a) Mzazi wa mwanachama au mzazi wa mwenza wa
mwanachama;
(b) Mtoto wa mwanachama wa kuzaa, kuasili au wa kambo
aliye na umri chini ya miaka ishirini na moja
(c) Ndugu wa damu wa mwanachama aliye na umri chini ya
miaka ishirini na moja.
38.
Swali:
Je, usajili wa mwanachama katika skimu ya bima ya afya utadumu kwa kipindi gani?
Jibu:
Usajili wa wanachama kutoka sekta isiyo rasmi katika skimu ya bima ya afya utadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
39.
Swali
Je, wananchi wasio na uwezo watapataje huduma za kijamii zilizofungamanishwa na bima ya afya kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia bima ya afya?
Jibu:
Wananchi wasio na uwezo baada ya kutambuliwa na Serikali watapatiwa vitambulisho maalum vitakavyowawezesha kupata huduma za afya na huduma zilizofungamanishwa bila mkwamo wowote.
40.
Swali:
Endapo kaya imechangia na hakuna mwanakaya aliyeugua katika kipindi cha mwaka mmoja wa uanachama wa bima ya afya, je kaya itarejeshewa fedha zake?
Jibu:
Hapana. Bima ya afya ni utaratibu wa kuchangiana ambapo kaya iliyopata wagonjwa na kutumia zaidi ya michango iliyotoa inachangiwa na kaya ambayo haijapata wagonjwa.Hivyo, wananchi wanaendelea kuhamasishwa kujiunga kwa kuwa ugonjwa unakuja bila taarifa.
Tags
Afya
Bima ya Afya kwa Wote
Bungeni
Habari
Makala
NHIF
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote
Wizara ya Afya