HIKI HAPA KISA CHA KUSISIMUA KUHUSU KIBALI CHA MATIBABU

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 2018 nilikuwa safarini natoka Dar es Salaam kwenda Mbozi, safari hii ilikuwa ya usiku kwa usiku kuwahi majukumu ya kiserikali katika Halmashauri ya Mbozi, mkoani Songwe.

Nilitoka Dar es Salaam jioni sana, mara baada ya kushiriki mazishi ya bibi yangu mzaa Baba Edwiki Binti Omari. Dereva aliyekuwa anaendesha gari la serikali nililokuwamo alikuwa mama mmoja wa Kindali anayefahamika kama Sofia.

“Mkuu tutakapofika Mikumi naomba tule chakula cha usiku na kuchimba dawa.” Nilijibu sawa maombi ya dereva huyu. Tulikaribishwa na taa nyingi za Mikumi usiku huo na gari letu kusimama kando ya mkahawa mmoja, tukala chakula na kuchimba dawa.

Mwanakwetu katika safari zangu zote nilipokuwa na dereva huyu nilibaini kuwa suala la uchimbaji wa dawa lilifanyika maeneo maalumu yenye mikahawa na hoteli na siyo vichakani kama desturi ya madereva wanaume. 

Hilo liliniaminisha kuwa kama Waswahili wanasemavyo siyo kila mti wa porini ni dawa, ndiyo maana dawa zinachimbwa katika miti maalumu.

Wakati tunarudi garini hapa Mikumi tuliposomama akaja ndugu mmoja akajitambulishwa kuwa yeye ni askari wa JWTZ kikosi kilichopo jirani na Mikumi na akieleza anakwenda nyumbani kwao Makambako kuzika anaomba msaada. Nikamuuliza unayo Movement Order ?

Ndugu huyu alitoa karatasi hiyo ikimtambusha, yeye ni askari wa cheo gani? Anatoka kikosi gani? Anatoka wapi na kwenda wapi? 

Hakuwa amevalia sare na hiki kikiwa ni kibali cha safari yake. Jamaa huyu alipanda gari hili na tukaanza safari ya usiku kucha tukiongea mengi mno safarini. Saa mbili ya asubuhi tulifika Makambako na ndugu huyu alishuka na sisi kunywa chai na kuendelea na safari ya Mbozi.

Dereva Sofia aliendesha gari tukiwa kimya hadi Igawa, tulipofika hapo akasema mkuu samahani, 

Eti uliwahi kupitia mafunzo ya JKT? Nikamjibu hapana. Akaniuliza swali lingine, Ulifahamia wapi MOVEMENT ORDER? Mwanakwetu nikacheka, alafu nikamuuliza umekumbuka pale nilipoiomba hiyo movement order ya yule askari aliyeshuka Makambako? Dereva akajibu ndiyo.

Nilimjibu hivi, “Yule bibi yangu tuliyemzika Mbagala jana alizaa watoto 10 wakiume mmoja ambaye ni baba yangu na wakike tisa, mabinti zake wanne waliolewa na askari au jamii watu wanaofanya kazi za namna hiyo. 

Wakati huo barua nyingi zilikuja nyumbani wakimjulisha babu/ bibi kuwa ‘Jamani tunangoja Movement Order tuje likizo’ huo ulikuwa msamiati uliotumika sana nyumbani kwetu lakini pia kwetu Mbagala pana kambi ya JWTZ tangu tunazaliwa, tunakuwa na hadi sasa tunazeeka msamiati huo ulitajwa mno. 

Askari ni watu wazuri sana, wana nidhamu sana, wachapa kazi sana pia hata katika ngazi ya familia. Hata wewe ukipata mchumba askari usimkatae utafaidi mno kama wanavyofaidi shangazi zangu.”

Mwanakwetu dereva Sofia aliendesha gari hilo vizuri sana na sasa tulikuwa Nanyara tukiitafuta Mlowo. 

Nikamwambia hata huu utaratibu wa askari wetu kutokulipa nauli katika daladala ni utamaduni uliyojengeka kutokana na heshima ya Watanzania wenyewe kwa askari wetu mara baada ya vita vya Kagera kumshinda Nduli Iddi Amin Dada. 

Watanzania wakawa wanasikia raha, wanaona fahari, wanakuwa salama kuwa jirani na askari hata kuwapakiza bure katika vyombo vya moto katika safari fupifupi, hilo ni jambo zuri sana nilimwambia dereva Sofia.

“Zamani waliitwa KAR-King African Rifles sasa ni JWTZ-Jeshi la Wananchi wa Tanzania, yaani ni jeshi la mimi na wewe.” Dereva Sofia aliendelea kupiga gia huku akitasamu na simulizi za mwanakwetu sasa tukafika Vwawa salama salimini.

Msomaji wangu kwa sasa tunaposema Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawa wanatoka katika jamii yetu ya Watanzania, anaweza akawa mtoto wako, anaweza akawa mjukuu wako, anaweza akawa shemeji yako, anaweza akawa kaka, anaweza akawa dada au anaweza akawa mmeoleana kama walivyokuwa wajomba wa mwanakwetu. Katika udugu huo hakuna siri yapo mengi ya kusimulia kama kisa hiki;

“… alipojifungua akapata matatizo ya ujauzito baada ya upasuaji, akapangiwa kufanyiwa upasuaji tena, akaambia angoje miezi sita ili mtoto anyonyenyonye kwanza, akifanyiwa upasuaji sasa mtoto atapata tabu, kweli alingoja miezi sita hali yake ikawa mbaya zaidi aliporudi hospitali zao akaambiwa atafanyiwa upasuaji, mtoto akabaki na nduguze. 

Akalazwa kitandani kwa upasuaji, akawekewa dripu, kanula na kaseta akapelekwa thieta kwa upasuaji. 

Akiwa thieta ikabainika kuwa kuna kifaa hakikuwepo kukamilisha zoezi hilo, zoezi likasogezwa mbele na mgonjwa akurudi nyumbani. Kifaa hicho kinauzwa shilingi 50,000/-, wakisema wataununua, mweza aliununua kwa pesa ya mfukoni mwake, siku zilisonga hakufanyiwa upasuaji…”

Jambo hilo liliikwaza mno familia ya mama mgonjwa wakisema hatutokubali ndugu yetu akipata shida na kwa nini asipelekwe Mloganzila? Hoja ilikuwa kibali cha matibabu hakiwezi kutolewa kwa kuwa ugonjwa huo wanauweza kuutibu katika hospitali yao, lakini mgonjwa tumbo lake lilikuwa linaharibika. 

Waswahili waliongea mno wakasema kama umeshindwa kumtunza mwanetu sisi tunaweza kumpeleka Mlongazila na hilo tukalifanya sisi. Mgonjwa alipelekwa hadi Mlongazila na nduguze,“Nipo tayari kumfanyia upasuaji mgonjwa wenu, alazwe leo na kesho nimfanyie huo upasuaji.”

Daktari Bingwa wa Mlongazila aliwahakikishia hilo. Mgonjwa alilazwa na kufanyiwa upasuaji na tamati ya yote alipona kabisa na hata sasa mama huyu anaweza kumzalia mtoto mwingine mpiganaji wetu. 

Kumbuka haya yalifanyika kwa malipo tasilimu ambapo mpiganaji huyu alilipa. Kwa hiyo ushauri wa ndugu zetu hawa kuweza kutibiwa katika hospitali zote za umma bila kibali ni muhimu kwani hata wao wanatusaidia mno Watanzania wengi katika hospitali zao.

Kwa hakika viongozi wa JWTZ wao wanaweza wakaona kuwa jambo hilo lipo katika mipango yao ya matibabu kwa askari wao, hilo sina ubishi nalo lakini wafahamu kuwa askari ni ndugu zetu wa damu na kuoleana pia, jambo hili linasumbua mno kama kisa hicho kilivyo. Wapo baadhi ya vijana hawa wana watoto wanaotibiwa kila mara wamejiunga na NHIF za miezi mitatu mitatu ili kuwanusuru watoto na wenza wao.

Mwanakwetu kisa hiki cha kibali cha safari kimenifanya nikusimulia kisa hiki cha kibali cha matibabu. 

Kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania ndiye Amri Jeshi Mkuu, yeye kama mzazi, yeye kama mama na yeye kama kiongozi alikague hili na kulifanyia kazi na mwanakwetu kwa heshima zote jambo hili nalipeleka machoni pake.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news