NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya shilingi bilioni 59.6 ili kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei za mafuta hapa nchini kwa wananchi na uchumi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati ya Maji (EWURA), Mhandisi Modestus M. Lumato.
Taarifa hiyo inaangazia kuhusu bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kuanzia Jumatano ya Oktoba 5, 2022 nchini.
"Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji EWURA), inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini, Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano ya Oktoba 5, 2022 saa 6:01 usiku.
"Bei za Mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kwa mwezi Agosti 2022 ambazo zimetumika katika kukokotoa bei za mafuta za hapa nchini katika mwezi wa Oktoba 2022 zimepungua kwa asilimia 7.4, 3.9 and 1.9 kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, mtawalia, ikilinganishwa na bei hizo kwa mwezi Julai 2022.
"Hata hivyo, ikilinganishwa na gharama za uagizaji zilizotumika katika kukokotoa bei za Septemba 2022, gharama za uagizaji wa mafuta zimeongezeka kwa kati ya asilimia 50 na 163 kwa kutegemea bandari na bidhaa husika ikilinganishwa na gharama za uagizaji zilizotumika katika kukokotoa bei za Septemba 2022, na hivyo kuathiri mwenendo wa bei za mafuta hapa nchini.
"Pamoja na hayo, kufuatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei za mafuta hapa nchini kwa wananchi na uchumi kwa ujumla, Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 59.58 kwa ajili ya bei za mafuta ya Oktoba 2022,"amesema Mhandisi Lumato.
Bei za rejareja zisizo na zenye ruzuku kwa Oktoba 2022
(Shilingi/Lita)
Aidha, kutokana na mgawanyo wa ruzuku kwa mafuta ya petroli na dizeli,jedwali hapa chini linaonesha ulinganisho kati ya bei zenye ruzuku za Septemba 2022 na bei zenye ruzuku za Oktoba 2022 kwa mujibu wa EWURA.
Bei kikomo za rejareja za Oktoba 2022 ukilinganisha na Bei kikomo za rejareja za Septemba 2022 (Shilingi/Lita)
Mhandisi Lumato amesema,bei kikomo za mafuta kuanzia Oktoba 5, 2022 ni kama zinavyooneshwa katika jedwali hapa chini.
Aidha,totauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bandari mafuta yanapochukuliwa na gharama ya usafirishaji.
Bei Kikomo za Mafuta tarehe 5 Oktoba 2022 (Shilingi/Lita)
Mhandisi Lumato amesema, katika kutekeleza bei hizi, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuzingatia yafuatayo: -
(a) Wafanyabiashara wa rejareja wa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) wanatakiwa kuchukulia mafuta Tanga na wafanyabiashara wa rejareja wa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) wanatakiwa kuchukulia mafuta Mtwara.
(b) EWURA inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
(c) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166,bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.
EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
(d) Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (Price cap) au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama ilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia Magazeti ya Serikali Na. 2A na 57 ya tarehe 3 Januari 2022 na 28 Januari 2022, sawia.
(e) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja.
Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.
(f) Wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na Wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia, risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.
(g) Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei yenye ruzuku kama inavyooneshwa kwenye Jedwali Na. 3. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka AGIZO hili.
(h) Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei yenye ruzuku kama inavyooneshwa kwenye Jedwali Na. 4. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka AGIZO hili.
JEDWALI NA. 3: BEI ZA REJAREJA (Shilingi/Lita)