Katibu Mkuu Mhandisi Sanga awauma sikio wahitimu Kidato cha Nne

NA MOHAMED SAIF

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewaasa wahitimu wa Kidato cha Nne kuwa mabalozi wazuri wa shule zao kitaaluma na kinidhamu ili kuwa mfano mzuri kwenye jamii wanayokwenda.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akisikiliza maelezo kutoka kwa wanafunzi wa Sekondari ya Mbalatse kuhusu namna ya kuchuja maji wakati wa mahafali ya kidato cha Nne.

Rai hiyo ameitoa kwa nyakati tofauti wakati mahafali ya shule za Sekondari za Lupila na Malatse Wilayani Makete Mkoani Njombe ambapo alishiriki kama mgeni rasmi.

“Kokote mtakapokwenda baada ya kuhitimu wakikuona unavaa vizuri unanyoa vizuri unasoma vizuri wakakuuliza umesoma wapi unakuwa unatangaza mema ya shule yako; mkawe raia wema huko,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akijadiliana jambo na baadhi ya wajumbe wa bodi na menejimenti ya Shule ya Sekondari Mbalatse wakati wa mahafali ya kidato cha nne.

Aidha, akiwa katika Mahafali ya 31 ya Kidato cha Nne ya Sekondari ya Lupila Oktoba 15, 2022, Mhandisi Sanga aliwashukuru viongozi wa dini, Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT) ambao ndio waanzilishi wa shule hiyo kabla ya kuikabidhi kwa Serikali mnamo mwezi Mei, 2001.

Katika mahafali hayo, wadau mbalimbali walishiriki na baadhi yao walipata fursa ya kutoa mawazo yao ya namna bora ya kuboresha hali ya kitaaluma ili kuiwezesha shule hiyo kung’ara zaidi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Lupila wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) wakati wa mahafali ya kidato cha nne.

“Tumepata mawazo mengi kutoka kwa wadau, tuendelee kujadili kuona vipi tutaboresha; mathalan mchango wa masuala ya kilimo, tutajadili kwa kina na kuishauri Serikali kutazama namna bora ya elimu ya kilimo kupewa kipaumbele kwenye mtaala wa shule,” amesema Mhandisi Sanga.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abkasa Ngwale aliishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboreshs Sekta ya Elimu kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu, vitabu, ruzuku kwa ajili ya chakula na ruzuku ya elimu bila malipo.

Awali akiwa kwenye Sekondari ya Mbalatse Oktoba 14, 2022, Mhandisi Sanga amewasisitiza kuepuka matokeo mabaya kwa kuongeza jitihada kwenye masomo yao na pia amewaasa wajifunze kwa jirani zao Shule ya Sekondari Lupila.

“Mnaweza kuanzisha kampeni ya kutokomeza zero, hili linawezekana kwa walimu, wanafunzi na wazazi; jirani zenu Lupila wanafanya vizuri jifunzeni kutoka kwao, nini wanafanya kutokomeza zero hadi kushika nafasi ya kwanza kimkoa,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alichangia fedha taslimu kiasi cha shilingi 1,000,000 ambayo alielekeza itumike kutatua baadhi ya kero zinazorudisha nyuma maendeleo ya shule hiyo.

“Nimesikia risala zenu sitoweza kutatua matatizo yote mliyoyasema kwa siku moja lakini tunaweza kusonga mbele kwa kushirikisha wadau,” amesema Mhandisi Sanga.

Aliwataka viongozi wa Kata ya Mbalache kushirikiana na wazazi kufanya jitihada za kutafuta wadau watakaosaidia kuchangia maendeleo ya shule yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news