NA DIRAMAKINI
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo
mezindua Chuo cha Ufundi Stadi na Duduma (VETA) Mkoa wa Kagera.
Ni chuo cha kisasa ambacho ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 22 ikiwa ni ufadhili kutoka Serikali ya China.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa
Kagera,Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
za Mkoa huo kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha asilimia 10 ya fedha
za mkopo kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu
zinawanufaisha pia wahitimu wa chuo hicho kwa kuwapatia fedha taslimu
au kuwanunulia vifaa na kuwatengea maeneo ili waweze kujiajiri.
Aidha,
Rais Samia amesema chuo hicho kina uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 1,400
wa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ambapo ameahidi kukipatia chuo
shilingi Bilioni 1 kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji ili kupunguza
makali ya ada huku akijitolea kusomesha vijana 20 ambao familia zao
hazina uwezo.
Ili kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo Cha
VETA,Rais Samia amesema Serikali itaendelea kutenga Shilingi Bilioni 100
kila mwaka kwa ajili ya Ujenzi wa Vyuo hivyo na kuhakikisha wilaya zote
62 ambazo hazina Chuo cha VETA zinakuwa na chuo hicho ikiwa ni pamoja
na ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Songwe.
Rais Samia amesema
lengo la ujenzi wa vyuo hivyo ni kuongeza thamani na ujuzi kwa vijana
wanaohitimu kuanzia Elimu ya Msingi mpaka chuo wapate ujuzi wa
kuwasaidia kujiajiri wenyewe ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa
ajira ambapo tafiti zinaonesha asilimia 12 ya vijana hawana ajira.
Kwa
upande wake Balozi wa China nchini Tanzania,Cheng Mingjian
amesema,ujenzi wa chuo hicho ni matokeo chanya ya ushirikiano baina ya
Serikali ya China na Tanzania katika mambo mbalimbali.
Chuo cha
VETA Mkoa wa Kagera kilichozinduliwa leo kina madarasa 19 na karakana 9
ambapo kitaanza kutoa mafunzo mwezi Januari, mwakani ambapo miongoni mwa
masomo yatakayofundishwa ni kompyuta, ufundi wa umeme wa majumbani na
viwandani, ufundi makenika, uchongaji vyuma, uchomeaji na uungaji vyuma,
ufundi bomba, ufundi umeme na mitambo, upakaji rangi, ujenzi, ufundi
seremala.