LEO Oktoba 31, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anazindua matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022. Hafla hii inafanyikia jijini Dodoma ambapo sensa hiyo ilifanyika mwezi Agosti, mwaka huu.
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.
Hivyo, Sensa ya mwaka 2022 ilikuwa ni Sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
WATANZANIA WAFIKIA MILIONI 64.7
Idadi ya watu nchini imeongezeka kwa asilimia 3.2 kwa miaka 10 iliyopita kutoka watu 44,928,923 mwaka 2012 hadi kufikia watu 64,741,120 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la watu 19,812,197.
Takwimu hizo zimetolewa leo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akizundua matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, takwimu ambazo zimeonesha idadi ya wanawake ikiwa kubwa zaidi kuliko wanaume kwa asilimia 51 na asilimia 49, mtawalia.
Takwimu nyingine zilizotolewa ni idadi ya majengo ambapo Tanzania kuna jumla ya majengo 14,348,372, vituo vya kutolewa huduma za afya vikiwa 10,067 (zahanati 7,089, vituo vya afya 1,490 na hospitali 688). Kwa upande wa elimu Tanzania ina jumla ya shule 25,626 ambapo shule za msingi ni 19,769 na shule za Sekondari ni 5,857.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wananchi, Rais Samia amesema zoezi la Sensa lilifuata vigezo vyote vya kimataifa, hivyo matokeo yanaweza kutumia popote duniani.
Ametumia jukwaa hilo kusisitiza kuwa takwimu hizo zitumike kuboresha maisha ya Watanzania kwani ndio lengo kuu, na kwamba Serikali imeandaa mwongozo wa matumizi ya matokeo hayo, ikiwa ni mwongozo wa kwanza kuandaliwa tangu uhuru, na mwongozo wa kwanza wa aina hiyo Afrika.
“Lengo kuu la mwongozo huu, ni kuongeza uelewa, uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka huu 2022 kwa wadau wote hususani Serikali katika kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na mazingira,” amesema Rais Samia Suluhu akiongeza kuwa “muongozo utetekelezwa kwa miaka 10 kuanzia Novemba 2022 hadi Oktoba 2032.”
Wakizungumza awali kuhusu Sensa ya mwaka 2022, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Kamisaa wa Sensa, Spika Mstaafu, Anne Makinda na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa wamewapongeza Watanzania na viongozi kila mmoja kwa nafasi yake kwa kufanikisha zoezi hilo ambalo litawezesha upangaji wa mipango ya maendeleo.