Maagizo ya Waziri Dkt.Mabula yawagusa wakurugenzi wote na wataalamu Sekta ya Ardhi nchini

ANTHONY ISHENGOMA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kujipanga na kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa ardhi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utendaji kazi na usimamizi wa sekta ya ardhi katika halmashauri.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika Kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 1, 2022. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dkt Allan Kijazi na kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe.

Dkt. Mabula alisema hayo leo Oktoba 1, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupata maoni juu ya muundo mpya wa utendaji kazi wa wataalam wa ardhi katika ngazi ya Halmashauri.

Dkt.Mabula alisema, zimeanza kujitokeza changamoto katika utendaji kazi kati ya watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa Halmashauri hasa katika eneo la usimamizi wa sekta hiyo baada ya kuanza utekelezaji wa rejesho la Waraka wa Utumishi Na 1 wa Mwaka 1998 kuhusu usimamizi wa watumishi wa sekta ya ardhi na maji kutokana na sababu mbalimbali.
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 1, 2022.

Rejesho hilo pamoja na mambo mengine liliwahamisha wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka kwenye usimamizi wa Mamlaka za serikali za mitaa Kiajira na kinidhamu na kuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi.

‘’Watumishi hawa kiajira na kinidhamu wako Wizara ya ardhi mamlaka za upangaji ardhi ziko Halmashauri lakini baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakijiweka mbali na wataalam ardhi na kushindwa kufuatilia utekelezaji wa sekta ya ardhi au kukosa ufahamu katika sekta ya ardhi,"alisisitiza Dkt.Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula changamoto hiyo imeleta mkanganyiko kwa kuwa baadhi ya watendaji hasa wakurugenzi hawaoni kama wanawajibu wa kusimamia sekta ya ardhi wakati wao ni mamlaka za upangaji ardhi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe akizungumza katika kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 1, 2022. Kushoto ni Waziri wa Ardhi Dkt.Angeline Mabula na kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Laurean Ndumbaro.

‘’Baadhi ya wakurugenzi hawajui taratibu za ardhi na kutojihusisha zaidi na uelewa wa masuala ya ardhi kwani unakuta Mkurugenzi wa Halmashauri ukimtaka hakupe taarifa anakimbilia kupata ufafanuzi kutoka kwa mtaalamu wa ardhi’’Aliongeza Dkt. Angeline Mabula.

Changamoto nyingine iliyoainishwa Dkt Mabula ni kitendo cha baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri kushindwa kurejesha fedha za mkopo ya program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi na kutumia fedha hizo kwenye mipango mengine badala ya kurejesha fedha hizo ili ziweze kutumika katika maeneo mengine.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akizungumza katika kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 1, 2022. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe na kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Laurean Ndumbaro.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi alieleza kupitia kikao hicho kuwa ipo haja ya kuboresha mawasiliano kati ya watendaji wa sekta ya radhi na mamlaka za serikali za mitaa ili kuweka mkakati mzuri wa utendaji kazi kwani wote ni watumishi wa Serikali.

Dkt. Kijazi aliongeza kuwa, kumekuwa na changamoto ya kiutendaji kati ya serikali za mitaa na uongozi wa kisiasa ikiwemo madiwani na kusisitiza kuwa, la msingi ni kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa wote ni watendaji wa serikali.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Halamashauri wakiwa katika Kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 1, 2022.

‘’Lengo la kikao chetu ni namna ya kuboresha mawasiliano ili tuweze kujiweka sawa kuboresha utendaji kazi kwani kumekuwepo lugha zinazoleta sintofahamu kuwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa wakitoa kauli kuwa watendaji wa sekta ya ardhi wako chini ya katibu Mkuu na wao hawahusiki,"amesema Dkt.Kijazi.

Madhumuni ya kikao kazi ni kujadili changamoto, kuibua changamoto zingine zinazojitokeza na kutoa maoni na ushauri kuhusu namna bora ya kusimamia watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuwa na ufanisi na kwa maskahi mapana ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news