Maonesho ya Madini kuchochea uwekezaji nchini,STAMICO kusaidia wachimbaji kukopesheka

NA TITO MSELEM

IMEELEZWA kuwa, Maonesho ya 5 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2022 yatachochea uwekezaji katika Sekta ya Madini na kuleta maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa Oktoba 3, 2022 na Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko wakati akifungua rasmi maonesho hayo yaliyoanza tarehe 27 Septemba, 2022 katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

“Napenda kuwashukuru wananchi na wadau wengine wakiwemo wawakilishi wa nchi mbalimbali walioshiriki maonesho haya ambayo ni tofauti na maonesho ya miaka mingine, mwaka huu kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi na wadau wengi wa madini kujitokeza kushiriki katika maonesho haya,"amesema Dkt.Biteko.
Dkt. Biteko amesema Maonesho hayo yatasaidia kuitangaza Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi pamoja na kuainisha fursa zilizopo nchini.

Aidha, Dkt. Biteko amesema Sekta ya Madini ni nguzo muhimu na kuwa ni chachu ya maendeleo kwa kuzingatia kuwa sekta hiyo inafungamanisha moja kwa moja na sekta nyingine za kiuchumi zikiwemo Sekta za Ujenzi, Viwanda, Kilimo, Usafirishaji na Mawasiliano.
Katika hatua nyingine, Biteko ametoa onyo kwa watoroshaji wa madini ambao wamebadili mbinu za utoroshaji kutoka kubeba dhahabu kwa kificho na kusafirisha kwenda nje ya nchi na sasa wanatorosha kwa kushusha ubora wa thamani ya dhahabu lengo likiwa ni kuikosesha Seriakli mapato.

“Wanaiba kisayansi wanashusha Purity ya dhahabu kama dhahabu ilikuwa ina asilimia 90, wanaishusha kuwa na asilimia 87 ambapo wanaondoa asilimia tatu, nataka niwaambie wanaofanya vitendo hivi kuwa wanatafuta mambo mawili, wanatafuta jela au umasikini,"amesema Dkt.Biteko.
Katika hatua nyingine, Biteko ameziomba taasisi za fedha kujenga imani kwa wachimbaji wadogo wa madini na kuwakopesha kwa kuwa sasa wameanza kuchimba kisayansi na kuwa Wizara yake kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ipo tayari kutoa taarifa ya uwepo wa madini kwa wachimbaji ili waweze kupewa mkopo.
“Mabenki yaliyoko hapa wameniambia wameshaanza kuwakopesha wachimbaji wamenieleza na kiasi walichokopesha nawatia shime ya kuwaamini kama wanastahili wakopesheni wapate mitaji waweze kuwekeza waaminini wachimbaji kwa sababu ni wafanyabiashara kama walivyo wafanyabiashara wengine,”amesema Dkt.Biteko.
Akizungumzia uharibifu wa mazingira unaofanywa na wachimbaji wa madini, amewataka maafisa madini na viongozi wa mitaa kusimamia mazingira ili kuokoa misitu inayoharibiwa na wachimbaji pamoja na wachoma mkaa na kusema Serikali inaendelea kutafuta teknolojia mbadala itakayotumiwa na wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Geita Martin Shigella amesema maonesho hayo yanaendelea kukua mwaka hadi mwaka na kwamba kunaongezeko la zaidi ya asilimia 50 ya washiriki wanaotoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, aliishukuru Serikali kwa kupunguza tozo kwa wachimbaji wadogo kwamba bado wanahitaji kujengewa mazingira mazuri ya mikopo ili waweze kukopa na kuchimba kisasa.
Alisema, ipo haja ya Sheria ya Madini kutazamwa upya ili dhahabu yote inayozalishwa iongezewe thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Pamoja na uwepo wa kiwanda kikubwa cha kusafisha dhahabu Mkoani hapa bado wachimbaji wanakwepa kupeleka dhahabu zao licha ya serikali kupunguza tozo kwa asilimia mbili kwa atakaepeleka dhahabu kwenye kiwanda hicho.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu alisema pamoja na sifa nzuri ya ukusanyaji mapato kutoka kwa wachimbaji wadogo ipo hatari ya eneo la Geita kugeuka jangwa kutokana na uharibifu wa mazingira ambapo ameiomba wizara kuingilia kati ili kunusuru uhalifu wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news