NA FRESHA KINASA
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Vision Ministries Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Safe Water Africa of Birmingham Alabama nchini Marekani wamekabidhi miradi ya maji safi na salama yenye thamani ya shilingi milioni 37.8 kwa makanisa saba yaliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara ili makanisa hayo yasimamie huduma ya utoaji wa maji safi na salama kwa jamii.
Makanisa yaliyokabidhiwa kusimamia miradi hiyo ni Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) lililopo Kata ya Kigera, Kanisa la Carivary Assemblies of God (CAG) lililopo Kata ya Buhare, Kanisa la Hope in Christ Church Tanzania (HCCT) katika Kata ya Kwangwa, Kanisa la Tanzania Gospel Church katika Kata ya Bweri (TGC), Kanisa la Evangelical Pentecostal Restoration Church (EPRC).Akizungumzia wakati wa kukabidhi miradi hiyo Oktoba 3, 2022 kwa viongozi wa makanisa hayo Mkurugenzi wa Shirika la Vision Ministries Foundation Tanzania, Joel Rugano amesema, kwa sasa wameifikia mikoa 19 hapa nchini na vituo 60 vinatoa huduma hiyo kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata huduma ya maji safi na salama ili kuondokana na magonjwa ya tumbo kama vile amoeba na homa ya matumbo ambayo yamekuwa changamoto kwa wananchi.
"Tunalenga kutoa huduma kwa jamii ikizingatiwa kwamba, watu wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa ya tumbo kutokana na kutotumia maji safi na salama. Sasa badala ya kuhangaika kutibu ugongwa sisi tukaona ni vyema kuzuia tatizo kwa kuweka miradi hii ambayo maji yake yanatibiwa kabisa kupitia mashine ya kisasa ambayo imekidhi viwango vyote kuhakikisha maji yanakuwa safi na salama kwa matumizi hii miradi tumeitoa bure ihudumie jamii chini ya usimamizi wa makanisa," amesema Joel Rugano.
Rugano ameongeza kuwa, kulingana na uhitaji ulivyo mkubwa kwa jamii wataendelea kusogeza huduma hiyo sehemu mbalimbali ambayo haijafikiwa zikiwemo taasisi kama shule, zahanati kwa kadri Mungu atakavyojalia kuwezesha upatikanaji wa fedha ili wananchi wengi waondokane na changamoto ya maji safi na salama katika kuunga mkono juhudi za serikali za kumtua ndoo mama kichwani.
Aidha, amesisitiza utunzwaji wa miradi hiyo kusudi iweze kudumu kwa muda mrefu na kusudi iendelee kuwanufaisha wanananchi kwani ndio shabaha kubwa kuhakikisha inakuwa na uendelevu na matunzo bora katika kuwasaidia Wanawake na watoto ambao hutumia muda mwingi kutafuta maji.
Kwa upande wake Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) lililopo Kigera Manispaa ya Musoma,Jacob Lutubija ambaye amepewa jukumu la kusimamia mradi huo amelishukuru shirika hilo na kusema kwamba wananchi wa Kata ya Kigera watanufaika na mradi huo kwa kupata maji safi na salama.
"Mbali ya kuwahudumia watu kiroho, lakini pia kanisa linawajibu wa kuwahudumia kimwili wapate mahitaji ya kawaida ni imani yangu kuwa mradi huu utawagusa watu wote bila kujalisha imani zao nalishukuru pia shirika kwa kutupa mradi huu ambao kwetu ni jambo la baraka na tutautunza udumu kwa muda mrefu,"amesema Askofu Lutubija.
Naye Joseph Shigemelo Mchungaji wa Kanisa la Calivary Assemblies of God CAG lililopo Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma amesema, mradi huo ni neema kubwa kwani mbali na kuwahudumia waamuni wa kanisa hilo utawanufaisha wananchi wa Kata ya Buhare ambao wanakabiliwa na changamoto.
"Maji haya yanatibiwa sote tumeshuhudia namna ya kutibu hii ni baraka kubwa kwetu kanisa na jamii inayozunguka kanisa kwani magonjwa kama Typhoid, na Amoeba yataweza kupungua kwa kiwango kikubwa kwa wananchi kwani watakuwa wakitumia maji safi na salama kupitia mradi huu,"amesema Mchungaji Shigemelo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Hope in Christ Church Tanzania lililopo Kata ya Kwangwa Manispaa ya Musoma, David Nyamita mbali na kulishukuru shirika hilo kwa mradi huo, amesema uhitaji bado ni mkubwa wa huduma hiyo hasa vijijini ameomba liangalie namna ya kupeleka miradi hiyo ya maji maeneo hayo kusaidia wananchi ambao wanatumia maji yasiyo safi na salama.
Julias Kasomi ni Askofu wa Kanisa la Tanzania Gospel Church (TGC) lililopo Mtaa wa Nyabisare Kata ya Bweri amesema, mradi huo utawasaidia wananchi kupata maji safi na salama na kuwaneemesha wananchi wanaozunguka mradi huo.
David Mrondoro ni Mchungaji wa Kanisa la Evangelical Pentecostal Restoration Church (EPCR) lililopo Kata ya Nyakato amesema, mradi huo utawasaidia wananchi wa kata hiyo kupata huduma hiyo ya maji safi na salama.
Mtendaji wa Kata ya Nyakato,Olivia Laurence amepongeza mradi huo na kusema utawanufaisha wananchi wote wa kata yake bila kujalisha dini zao.
Neema Mathias Mkazi wa Kata ya Nyakato ameieleza DIRAMAKINI kuwa, huduma ya maji safi na salama ni muhimu katika kuchochea maendeleo na uzalishaji hasa kwa kina mama na watoto na hivyo ameshukuru mradi huo kuwepo katika kata hiyo.