NA MWANDISHI WETU
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amemuondoa kwenye majukumu yake aliyekuwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero kwa kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ikiwemo ujenzi wa Boksi Kalavati katika Barabara ya Mawala-Mofu-Ikwambi kilomita 30 iliyopo Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

“Nimekagua na kujiridhisha kwamba mradi huu umejengwa chini ya kiwango, kwakweli sijaridhishwa kabisa na usimamizi wa hapa, hivyo nimemuondoa kwenye nafasi yake kuanzia leo aliyekuwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero na atapangiwa majukumu mengine,”amesema Mhandisi Seff.

Pia, Mhandisi Seff amewataka Mameneja wa TARURA nchi nzima kusimamia kikamilifu miradi kwenye maeneno yao na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atayeshindwa kutimiza majukumu yake ili kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali inaendana na ubora wa miradi inayotekelezwa.