NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesisitiza haja ya kuwa na chombo maalum cha kusimamia utekelezaji wa mapendekezo na mageuzi ya kweli, juu ya namna ya kuyafikia maridhiano ya dhati ya kisiasa hapa nchini.
Mheshimiwa Othman ametoa msisitizo huo leo Oktoba 6,2022 wakati akifunga Mkutano wa Kujadili Masuala Mahsusi ya Zanzibar Yanayohusu Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Amesema kuwa, chombo hicho kitaweza kuratibu na kusimamia dhamira ya dhati ya utekelezaji wa maazimio na mapendekezo yaliyowasilishwa na wajumbe wa mkutano huo sambamba na matakwa ya wananchi wema, ili kuhakikisha ufanikishaji wa demokrasia na maridhiano ya kweli ya kisiasa hapa nchini.
Mheshimiwa Othman ametilia mkazo uwepo wa chombo hicho ambacho kitapelekea dhamira ya kutekeleza kwa vitendo, demokrasia ya kweli ili isitikiswe wala kuyumbishwa na changamoto za ndani au nje ya mirengo ya kiitikadi, pamoja na kuhimiza umuhimu wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuweka misingi imara kwa ajili ya ujenzi wa Zanzibar mpya.
Akisisitiza dhamira iliyotajwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi, wakati wa Ufunguzi wa Mkutano huo, Mheshimiwa Othman amesema kuna ulazima wa kuendesha Nchi kwa kuzingatia misingi inayoakisi maendeleo ya dunia ya leo.
Amesema kwamba, Wazanzibari wanahitaji kuwa na mtazamo unaofanana katika dhamira na ulazima wa mamabadiliko ya kifikra, kisiasa na kiuchumi, vinginevyo itakuwa ni vigumu kujenga demokrasia na kufikia mageuzi ya kweli.
“Dhamira ya dhati inapimwa na matendo yakila mmoja wetu, hivyo hayo yote tuliyoyaazimia yanapaswa kuwekewa utaratibu wa namna bora ya kuyatekeleza, Kila Mzanzibari anastahiki kufahamu kipi kitafanywa lini na nani; ni kwa namna hii tu ndio tutaondosha kulaumiana na kutiliana shaka kwani wahenga wanatuambia siku zote kuwa Matendo ni fasaha Zaidi kuliko maneno,”ameeleza Mhe.Othman.
Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuyatafakari, kuyazingatia na kuyatendea-kazi mambo yote ya msingi yaliyojiri hapo, na kuazimia kufanikisha utekelezaji wa dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi, kama ambavyo Viongozi Wakuu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameshaonesha dira.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Mhe. Hamza Hassan Juma, ameshukuru juhudi za Viongozi Wakuu wa Nchi, katika kufanikisha Mkutano huo ambao, unachukuliwa kuwa ni hatua muhimu katika ujenzi wa demokrasia hapa Visiwani, akisema anaamini mawazo na michango iliyowasilishwa itasaidia katika kuleta mageuzi ya kweli.
Akieleza mafanikio na ufanisi katika uendeshaji, sambamba na mijadala iliyoendeshwa kwa kuzingatia kanuni, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Dokta Ali Ahmed Uki, ametaja mada mbalimbali zilizowasilishwa hapo kuwa ni: Historia ya Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa Zanzibar; Uzoefu kutoka kwa wanasiasa kuhusu masuala mahsusi ya Zanzibar yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa; na Umuhimu wa uzalendo, uadilifu, kuheshimu Sheria, kudumisha amani na utulivu katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na kujenga uchumi endelevu wa Zanzibar.
Mkutano huo wa Siku Tatu, ambao umeratibiwa kwa mashirikiano ya Ofisi ya Rais wa Zanzibar, pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, sambamba na Washirika mbali mbali wa Maendeleo, umewajumuisha Viongozi wa Serikali, Tume za Uchaguzi; Vyama vya Siasa, Dini na Asasi za Kiraia; Majaji na Wanasheria; wakiwemo Makamu wa Pili Mstaafu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi; na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi.