NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema diplomasia ya nje inahitaji kutumika vyema ili kujenga uelewa, kwaajili ya kufungua fursa zaidi za maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa diplomasia ni njia muhimu na inayoweza kutumika kuibua fursa zinanazopatikana katika Jamii ya Kimataifa na Nchi za Kigeni, pindipo itatumika vyema katika kujenga uelewa kwa watu, taasisi na hata Serikali, ili kufanikisha njia mbali mbali za kujiletea maendeleo, bali kwa Tanzania na hata Mataifa mengine Barani Afrika, huenda hawajaitumia vyema nafasi hiyo.

Ametolea mfano fursa zinazopatikana kupitia Jumuiya ya Kimataifa ya Haki Miliki za Kitaalamu (WIPO) ambayo yeye amewahi kuitumikia hapo kabla, akiwakilisha Mataifa ya Afrika.

Naye Waziri Tax, amesema kuwa yupo tayari kwaajili ya kazi ya kuitumikia Nchi katika kujenga uelewa kupitia diplomasia, sambamba na kuhakikisha ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya Mambo ya Muungano, sambamba na fursa mbali mbali, zikiwemo za Maazimio yanayopitishwa mbele ya Jamii na Jumuiya za Kimataifa.
Waziri huyo ambaye ameteuliwa kushika wadhifa huo kupitia hatua ya hivi karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kulifanyia mabadiliko madogo Baraza lake la Mawaziri, ameahidi kutekeleza na kuyafanyia-kazi maagizo na miongozo yote, katika kuhakikisha Taifa linafaidika kupitia diplomasia ya nje.