NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ili kujenga Taifa imara, ni wajibu kuweka misingi bora ya kuwaandaa wasomi wenye weledi watakaoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko kwa ajili ya zama zijazo.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Oktoba 22, 2022, akiwa Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, huko katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi unguja.
Amesema kuwa, wakati huu ambao jamii inaelekea katika mjadala mkubwa wa mageuzi ya sekta ya elimu, na iwapo kuna umuhimu wa kujenga hatima njema, taifa imara na kizazi kilichotayarishwa kukabiliana na changamoto za zama zijazo, ni wajibu kuwa na tafakuri ya dhati, ya wazi na yenye upeo stahiki.
Mheshimiwa Othman amesema kuwa ili kuenzi dhamira ya dhati na maono ya Marehemu Maalim Seif, katika kujenga Zanzibar na Tanzania Mpya, huru, yenye uchumi imara, amani na maridhiano, safari inaanzia na uhuru katika Sekta za Elimu na Jamii, zinazojali ukuzaji wa vipaji, ubunifu na uwezeshaji.
Aidha, Mheshimiwa Othman akieleza umuhimu wa Taasisi ya Maalim Seif sambamba na Mkutano huo amesema, “Taasisi inatoa fursa muhimu ya kuwaleta wananchi pamoja na kujadili, kubadilishana mawazo na kuendeleza misingi ya kitaifa bila kujali itikadi wala misimamo; kwa hakika ni nyenzo muhimu ya ujenzi wa Taifa”.
Akiwasilisha Mada kuhusu Mjadala wa Kidunia Juu ya Elimu Sahihi kwa Watoto Werevu, Mheshimiwa Othman amefafanua kwa kusema, “katika hili ni vyema kueleza mapema kwamba watoto werevu wamekusudiwa ni wale waliotayarishwa kukabiliana na changamoto za sasa na tunakoelekea katika maisha kwa ujumla wake”.
Katika Mada yake, licha ya kubainisha kuwa suala la ubora wa elimu na watoto weledi, ni kitendawili kigumu kukitegua, bali yapo mambo ya msingi ambayo jamii inawafiki kuyazingatia ili kufikia mafanikio zaidi.
Mafanikio ambayo ni pamoja na Elimu ya Dini, maadili, aina ya wazazi na walezi, makuzi, mazingira ya kusoma, nafasi na hadhi ya mwalimu, mwanafunzi, mitaala, mfumo wa usimamizi wa ubora wa elimu na aina ya uchumi wa nchi kwa jumla.
Pia utayarishaji wa wanafunzi kuwa na upeo wa kufikiri na kutumia elimu katika mazingira yao badala ya kukariri; uandaaji wa wanafunzi kuwa wabunifu; na utayarishaji wanafunzi kuwa na uwezo wa kuwasiliana na kuwasilisha mawazo yao ikiwemo kutathmini na kuhoji.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maalim Seif, Bw. Ismail Jussa Ladhu, ameeleza kwamba katika Maadhimisho ya Mwaka huu, wameamua kwenda sambamba na yale aliyoyatarajia Mwanaharakati huyo maishani mwake, yakiwemo Maudhui Bora ya Elimu.
Naye, Mwanazuoni na Mwanataaluma Mashuhuri, Profesa Issa Shivji, akitilia mkazo dhamira ya Marehemu Maalim Seif katika kupigania haki, ameitaka Taasisi hiyo kumuenzi Kiongozi huyo kwa kuzingatia maono muhimu ya Haki na Uhuru, katika Sekta za Elimu na Jamii.
Wengine waliopata fursa ya kuwasilisha Salamu zao za Kumuenzi Marehemu Maalim Seif, ni pamoja na Balozi Didier Chassot (wa Uswisi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania); Mhe. Regina Hess (Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Nchini Tanzania);
Bi. Inge Herbert (Mkurugenzi wa Eneo la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara – ‘Friedrich Naumann Foundation for Freedom’); Jorunn Maehlum (Balozi Mstaafu wa Norway, Nchini Tanzania);
Bw. Mark Green (Balozi Mstaafu wa Marekani, Nchini Tanzania); na Bw. Roeland van de Geer (Balozi Mstaafu wa Umoja wa Ulaya (EU) Nchini Tanzania), ambao wote wamemkumbuka Marehemu Maalim Seif kuwa Mtu wa pekee, jasiri, mpambanaji na ambaye hakukata tamaa hadi mwisho wa maisha yake.
Kaulimbiu ya Mkutano huo wa Pili, wa Siku Mbili, ambao umeandaliwa na Taasisi ya Maalim Seif (Maalim Seif Foundation) kwa mashirikiano na Jumuiya mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa, ni Elimu na Ukuzaji Vipaji, Ubunifu na Uwezeshaji.
Viongozi wa Serikali, Dini, Vyama vya Siasa, Mawaziri na Mawaziri Wastaafu, Wasomi na Wanataaluma, wakiwepo pia Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali; Wachambuzi wa Siasa za Kitaifa na Kimataifa, Bw. Ahmed Rajab kutoka Uingereza, Bw. Hamza Kasongo kutoka Dar es Salaam; Balozi Ali Abeid Karume; Bw. James Mbatia; Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa; Sekta Binafsi; Asasi za Kiraia; na Wanadiplomasia mbali mbali kutoka ndani nje ya Tanzania, wamehudhuria katika Mkutano huo.
Wengine waliohudhuria hapo ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Mhe. Zitto Zuberi Kabwe; Mjane wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Bi Awena Sinani Masoud; na Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib.