NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza haja ya kuwaenzi na kuwathamini wazee, kuwa ni mwendelezo wa utamaduni uliowachwa na viongozi waliopigania ukombozi wa nchi, ili kujenga ustawi bora wa jamii.
Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, ameyasema hayo leo, kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wazee pamoja na familia mbalimbali alizotembelea katika ziara yake maalum visiwani hapa.



Miongoni mwa Wazee waliotembelewa katika ziara hiyo, Mzee Hamad Salim (79) Mkaazi wa Magomeni Kwa-Najim, ametoa wito kwa Viongozi wa Serikali na Vyama Siasa kuendelea kuijali rika na sehemu hiyo muhimu ya jamii.
Amesema kuwa, wazee wa hapa visiwani wameutumia umri wao mwingi katika kupigania Mamlaka ya Nchi bila ya kukata tamaa, hivyo ni wajibu wa viongozi waliopo madarakani sasa, kuendeleza jukumu hilo “kwa kuendelea kutweka tanga hadi pale jahazi litakapofika ufukweni kwa salama na mafanikio zaidi”.
Masheha na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, na Vyama vya Siasa, akiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Bw. Salim Bimani, wameambatana na Mheshimiwa Othman, katika ziara hiyo.