Miaka 23 bila Mwalimu Nyerere,haya hapa mambo aliyopenda kuyasisitiza

NA DIRAMAKINI

APRILI 13, 1922 alizaliwa mtoto shujaa na hodari kutoka katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara.
Si mwingine bali ni Julius Kambarage Nyerere. Alikuwa mmoja wa watoto 26 wa Chifu wa kabila la Wazanaki, Mzee Nyerere Burito.

Alipokuwa mtoto,Julius alichunga mifugo ya baba yake na alipofikisha umri wa miaka 12 alianza shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma Shule ya Wamisionari Wakatoliki huko Tabora.

Alipofikisha miaka 20, alibatizwa akawa Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake. Mapadre walibaini kipaji alichonacho wakamsaidia kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 hadi 1945.

Akiwa Makerere alianzisha Tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika na pia akajihusisha na Tawi la Tanganyika African Association (TAA).

Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akawa Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya St. Mary´s. mwaka 1949 alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uingereza akasomea Shahada ya Uzamili ya Historia na Uchumi.

Alihitimu mwaka 1952. Alikuwa Mtanzania wa kwanza kusoma katika Chuo Kikuu cha Uingereza na Mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.

Julius Kambarage Nyerere aliporejea Tanganyika kutoka masomoni alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika Shule ya Sekondari ya St. Francis (Dar es Salaam) ambayo kwa sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Tanganyika African Association (TAA),chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Mwaka 1954 alikibadilisha Chama cha TAA kuwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko cha TAA.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Chama cha TANU tayari kilikuwa chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika. Uwezo wa Mwalimu Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha achague kufanya kazi ya siasa au abaki na kazi ya ualimu. Julius Kambarage Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Hivyo, alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika kupigania Uhuru.

Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la Udhamini na Kamati ya Nne ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani.

Uwezo wake wa kuunganisha watu ili wawe na umoja na mshikamano kutetea haki zao pamoja na kipaji chake cha kujenga hoja, kutetea na kuzungumza kwa ufasaha ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata Uhuru bila umwagaji wa damu.

Ushirikiano mzuri aliouonesha kwa aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Bw. Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa Uhuru.

Uongozi

Tanganyika ilipata Uhuru wake Desemba 9, 1961 na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru. Mwaka mmoja baadaye, Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.

Aidha, Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika kuleta Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyounda Tanzania baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ambayo yalimtoa madarakani Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

Februari 5, 1977 Mwalimu Nyerere aliongoza chama cha TANU katika kuungana na chama tawala cha Zanzibar cha Afro - Shiraz Party (ASP) na kuanzisha Chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Mwenyekiti wake wa kwanza.

Mwalimu Nyerere aliongoza Taifa kwa miaka 23 hadi mwaka 1985 alipostaafu na kumwachia nafasi Rais wa Awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Yeye alibaki kuwa Mwenyekiti wa CCM hadi mwaka 1990 alipostaafu licha ya kuwa aliendelea kuwa na heshima kubwa katika nyanja za siasa ya Tanzania na duniani hadi kifo chake.

Mwalimu Nyerere alitumia muda mwingi kukaa kijijini kwake Butiama huku akilima shambani kwake. Pamoja na hayo, alianzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation mwaka 1996.

Aidha, alikuwa mpatanishi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi. Pia kati ya mwaka 1987 hadi 1990 alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini (South Commission).

Mauti

Oktoba 14, 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St.Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu.
Mwili wa Mwalimu ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani.

Oktoba 20, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao.

Aidha,Oktoba 21, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo. Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi Oktoba 22, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya maziko.

Maziko ya Mwalimu Nyerere yalifanyika Oktoba 23, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika Kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara.

Muhimu

Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alikua akiamini katika falsafa ya Ujamaa na kujitegemea. Hayati Mwalimu Nyerere alifanya hotuba mbalimbali katika mikutano ya ndani na nje ya nchi wakati wa uongozi wake na hata baada ya kustaafu.

Miongoni mwa mambo ambayo alipenda kuyasisitiza katika hotuba zake enzi za uhai wake mara kwa mara akiwa katika shughuli zake na hata mikutano au hotuba ni pamoja na ukabila,dini,ujinga,uongozi na muungano.

Ukabila

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake suala la ukabila alilikemea kwa nguvu zote na alihakikisha jamii zinaishi kwa umoja, mshikamano na upendo.

Aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake kupitia mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995 kuwa, ''nilikutana na mama mmoja akaniambia alikua akifanya kazi Jumuiya ya Afrika Mashariki, na sisi watu wa Uganda tulikua tunajuana kwa makabila yetu, watu wa Kenya walikua wakijuana kwa makabila yao, huyu Mkikuyu, huyu Mluhya.

"Lakini sisi Watanzania hatujui makabila ya watu, nikawambia mama ni wakati huo, sasa hivi watanzania wanataka kujua makabila yao, ya nini, mnataka kutambika? Majirani zetu waalikua wanaiga kutoka Tanzania, sasa bila haya na sisi tunataka kuulizana makabila?

Mwalimu Nyerere alikemea suala la ukabila kila wakati alipopata nafasi ya kuzungumza na hakutaka kabisa kuwe na maswali kama wewe ni kabila gani? Na katika hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, si kwa kawaida hapa nchini kuulizana kuhusu masuala ya ukabila.

Dini

Jambo ambalo alisisiza sana katika hotuba zake, hasa kuwaasa viongozi wasitafute uongozi kwa kutumia dini.Aliwahi kusema ''mambo haya ya kuchochea chuki za dini yakianza na tukayapa nafasi hayana simile, ni ikifika wakati yakashika kasi hakuna wa kuzuia."

Ujinga, maradhi na umaskini

Pia Mwalimu Nyerere alisisitiza juu ya mambo haya makuu matatu, na aliongeza pia kama Tanganyika na baadae Tanzania itafanikiwa kuyamaliza basi itakua miongoni mwa nchi itakayoendelea zaidi duniani.

Katika suala la kupinga umaskini Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ''nchi hii ni bado ya wakulima na wafanyakazi, hatuwezi kuwa nchi ya watu wenye kudai na kudai, nawaomba ndugu zangu watanzania hatujalemaa sana, lakini kilema kipo, viongozi wetu wanadai na kudai tuu, watu ni maskini, wachache hao wana nguvu ya kuongoza nchi hii ndio wanaodai tuu''.

Uongozi

Aidha, katika suala la uongozi, maadili ya uongozi ni jambo ambalo Mwalimu Nyerere aliliweka mbele sana, miongoni mwao ni viongozi ambao wanaweza kukidhi matarajio ya watanzania.

Nukuu mojawapo ya hotuba yake akizungumzia uongozi ni, ''Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM, inatakiwa ukiulizwa swali kwamba huyu atapiga vita rushwa? Jibu litoke ndani ya moyo, nchi yetu ni maskini bado haijawa ya matajiri hivyo tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wetu na matatizo ya wananchi, tunataka nchi yetu ipate kiongozi safi''.

Muungano

Wakati huo huo, katika vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alikua akitamani sana kufanya ni kuunganisha nchi za Afrika Mashariki, na kuwa na uongozi wa pamoja, ingawa hakufanikiwa katika hilo, alifanikiwa katika kuunganisha Tanganyika na Zanzibar mwaka 1994.

"Matumaini yangu, ilikua kuunganisha nchi hizi za Afrika Mashariki na kuwa muungano mmoja, kwa upande wa Zanzibar niliongea na Karume (Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Abeid Karume), akasema niko tayari ita watu wa magazeti sasa hivi, nikamwambia tufanye taratibu na tukafanikiwa. Kwa Afrika Mashariki tungekua na serikali tatu za kila nchi na serikali ya muungano yani ya Tanganyika na muungano''.

Mbali na hayo, Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao waliachia madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda wa miaka 23.

Pia alileta umoja, upendo, mshikamano, amani na haki Tanzania na barani Afrika na alishiriki hatua mbalimbali za kupigania hadi kupata Uhuru.

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alitokomeza ubaguzi wa rangi,kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni Mwalimu. Kazi hii ndiyo ilimpatia jina maarufu la Mwalimu.

Alijenga umoja wa Taifa na utamaduni wa Kiafrika pamoja na kukuza lugha ya Kiswahili na alitetea usalama wa Taifa katika vita dhidi ya Nduli Idd Amin.

Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa kwa Vyama vya Ukombozi vya Nchi za Kusini mwa Afrika kama vile ZANU (Zimbabwe), ANC na PAC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia), MPLA (Angola) na FRELIMO (Msumbiji).

Alisimamia sera za kujali utu na ubinadamu, alikuwa Muasisi wa itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha. Azimio hilo lilikuwa na shabaha ya kujenga nchi ya Kijamaa ambayo watu wake ni huru na wenye uwezo wa kuamua mambo yao wenyewe.

Vile vile, Mwalimu Nyerere alikuwa Muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na alikuwa Muasisi wa Chama cha TANU na CCM ikiwemo OAU na South South Cooperation.

Kinana asema

Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ametaja mambo manne ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akiyasimamia enzi ya uhai wake kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Akifungua Mdahalo huo Uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Uliokutanisha vyama rafiki vya ukombozi Kusini mwa Afrika, Viongozi mbalimbali pamoja na Wanazuoni, Kinana amesema falsafa ya Mwalimu Nyerere ilijengwa na misingi imara kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania na Bara la Afrika kwa Ujumla.

"Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na maono ya kujua Uelekeo wa Taifa na wapi Watanzania wanatakiwa kuelekea na hiyo ilitokana na msimamo wake na kutotetereka,” amesema Kinana.

Kuhusu suala la Uadilifu, Kinana amesema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na misingi ya uadilifu na kwa kujali aliokuwa akiwaongoza ambapo alipenda Uongozi Shirikishi.

“Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na Ushawishi mzuri kwenye Chama na Serikali na hiyo ilisababishwa na uwezo wake mkubwa wa Kujenga hoja kwa ajili ya maslahi ya aliokuwa akiwaongoza,” amesisitiza Kinana.

Kimiti

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Paul Kimiti ameomba watanzania kuyaendeleza yale yote mema yaliyofanywa na mwalimu ili kulijenga taifa katika misingi imara ya upendo mshikamano na umoja zaidi.

Chijoliga

Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Maselino Chijoliga amewakaribisha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kwenda kusoma kozi fupi za uongozi zilizopo katika chuo hicho ili ziwajengee uwezo wa kuongoza vyema kwa maadili ya uzalendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news