NA VERONICA MWAFISI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) inasaidia kujenga afya za watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao vema na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akicheza netiboli katika uwanja wa Bandari jijini Tanga wakati wa Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI).

Mhe. Jenista amesema hayo, wakati akifungua rasmi Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) kwa mwaka 2022 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, iliyoanza Oktoba 1, 2022 na inatarajiwa kufikia tamati Oktoba 15, 2022.
Ameongeza kuwa, kutokana na umuhimu wa michezo ya SHIMIWI, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alielekeza kurejeshwa kwa michezo ya SHIMIWI ili itumike kujenga afya ya akili na mwili kwa watumishi wa umma nchini, maelekezo ambayo yalitolewa na Mhe. Waziri Mkuu wakati akimuwakilisha Mhe. Rais Samia kwenye mbio za hisani zilizoandaliwa na benki ya CRDB.

“Sitegemei kusikia kuna mtumishi yeyote amejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu kwani michezo ya SHIMIWI ni sehemu ya kazi,” Mhe. Jenista amesisitiza.
“Ni matumaini yangu kuwa, michezo hii itaendeshwa kwa kuzingatia nidhamu, weledi na viwango vya hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali,” Mhe. Gekul amesisitiza.
Naye, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa watumishi wa umma na kuridhia watumishi wa sekta zote kushiriki michezo ya SHIMIWI kwa ajili ya kujenga afya.
Sanjari na hilo, Bw. Mwalusamba, amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa kufungua michezo hiyo muhimu inayowakutanisha watumishi wa umma kutoka katika Wizara, Mikoa, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali ambao wananufaika na michezo katika kujenga afya zao.
Zaidi ya watumishi 1000 wanashiriki michezo ya SHIMIWI mwaka huu inayojumuisha soka, netiboli, riadha, kuvuta kamba, bao, kurusha tufe, karata, mbio za baiskeli pamoja na drafti na yenye Kaulimbiu “Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na huongeza tija mahala pa kazi…..Kazi Iendelee”.