NA FRESHA KINASA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana amesema, wizara hiyo inaendea kutangaza vivutio na maeneo mbalimbali ya utalii nchini kupitia njia mbalimbali ikiwemo michezo, mikusanyiko na matamasha katika kuhakikisha kwamba taifa linapiga hatua kimaendeleo kupitia utalii wa ndani na utalii wa wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja nchini.
Ameyasema hayo leo Oktoba Mosi, 2022 wakati wa kuhitimisha mbio za hiari za Mwalimu Nyerere Marathoni zilizofanyika Butiama mkoani Mara zilizokuwa na lengo la kumuenzi na kutangaza urithi wa Mwalimu Nyerere ambaye ni mwasisis wa Taifa la Tanzania ambaye pia alitoa mchango wa ukombozi wa mataifa mbalimbali barani Afrika.
Mbio hizo zilikuwa katika makundi ya kilomita nne, kilomita13 na kilomita 22 ambapo kauli mbiu ya ilikuwa inasema 'Talii Kiutamaduni', jenga na piga hela' ambapo Waziri Chana na Naibu Waziri wa wizara hiyo pamoja n viongozi mbalimbali wa Wizara na Serikali wameweza kushiriki mbio hizo.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Chana amesema kuwa, watalii wengi wanaongezeka kuja nchini kutona na uongozi bora na siasa safi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba mchango wa Filamu ya Royal Tour imesaidia kwa kiwango kikubwa kulitangaza Taifa la Tanzania na vivutio vyake kimataifa na hivyo kuongeza idadi ya watalii wengi nchini.
Ameongeza kuwa, sekta ya utalii nchini ina umuhimu mkubwa katika kuleta maendeleo kwa watanzania, hivyo wizara hiyo itaendelea kutekeleza majumumu yake kwa ufanisi katika kuhakikisha maeneo na vivutio vyote vinatangazwa kwa ufanisi kuvuta watalii wa ndani na watalii wa nje kuja nchini.
Waziri Dkt.Chana amesema, Mwalimu Nyerere Marathon ni moja ya mpango wa wizara hiyo kuutangaza Utalii wa Tanzania na hivyo amesema kuwa mbio hizo zinaendelea kufanyika kila mwaka na kuiboreshwa zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mary Masanja, ametoa rai kwa Watanzania wote kupenda michezo ili kuimarisha afya kwa kuondoa magonjwa nyemelezi na pia kuchangia kuhamasisha michezo kupitia mbio mbalimbali.
Amesema, mbio hizo zimeadhimisha kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo na kwamba kitendo hicho ni muhimu sana. Huku akisema kumbukumbu hizo zitazidi kuenziwa kwa faida ya Watanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Makumbusho ya Taifa,Dkt.Osward Masebo akisoma risala amesema kuwa, lengo la marathoni hiyo ni kuenzi na kutangaza urithi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na mbio hizo zimeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Makumbusho ya Taifa kwani imepewa dhamana ya kutafiti, kukusanya, kuhifadhi na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na urithi wa asili na utamaduni.
Ameongeza kuwa, Watanzania wanapaswa kukumbuka kwamba maisha, utumishi na upekee wa Mwalimu Nyerere ni mojawapo ya urithi mkubwa wenye thamani kwa taifa, Afrika na Dunia kwa ujumla.
"Kupitia mbio hizi za hiari, inawakumbusha kwamba Watanzania Mwalimu Nyerere amebeba utambulisho wetu, urithi wetu, hatua zetu kama taifa, upekee wetu kama taifa, kumbukumbu yetu kama taifa. Moja ya mambo yanayoleta utamu katika historia hii ya Taifa letu ni upekee wa maisha ya Mwalimu Nyerere,"amesema Dkt. Masebo.
Pia, mbio hizo za Mwalimu Nyerere ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa miaka 10 ya kuenzi na kutangaza urithi wa Mwalimu Nyerere uliozinduliwa na Waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda tarehe 13, Aprili 2022 wilayani Butiama mkoani Mara wakati wa sherehe ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere.
"Kuna mambo matatu ya kufurahisha katika kutekeleza mpango huu kwanza Makumbusho ya Taifa tunapata nafasi ya kushirikiana na wadau wetu kutangaza urithi wa Mwalimu Nyerere kitaifa na kimataifa, pili Makumbusho inatumia maadhimisho haya kutangaza bidhaa mpya ya utalii wa michezo.
"Kilomita za kukimbia zimegawanyika kulingana na tarehe, mwezi aliozaliwa yaani tarehe 13,04, 1922 wapo waliokimbia kilomita 13 hiyo ni tarehe aliyozaliwa, wapo waliokimbia kilomita 4 huo ni mwezi aliozaliwa, wapo waliokimbia kilomita 22 hiyo ni kumbukumbu mwaka aliozaliwa,"amesema Dkt.Masebo.
"Kuna jambo jingine la kufurahia sana yaani barabara ya kutoka Busegwe kwenda Butiama iliyotumika kwa mbio hizi, ndio njia aliyokuwa anaitumia Mwalimu Nyerere kutoka nyumbani kwenda shuleni au kutoka shuleni kurudi nyumbani wakati akisoma shule ya Msingi Mwisenge Musoma,"amesema Dkt.Masebo.
Aidha, amewataka Watanzania kutambua kwamba Makumbusho ya Taifa imebeba na inashughulika na historia ya Tanzania na mahusiano ya Tanzania na Jamii za nje ya Tanzania, inashughulika na Utamaduni wa Taifa, inashughulika na ujenzi wa misingi ya taifa, kutunza na kilinda utamaduni, usalama kama nchi, hatima ya ustawi wa taifa, utamaduni wa Taifa, utaifa wetu, kumbukumbu zote zinazolinda taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, amesema mbio hizo zimechangia katika kuchochea uchumi wa wakazi wa Butiama na kuchocheo uchumi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Mara kwa ujumla.
Neema Peter ni mkazi wa Butiama amesema kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi bora na mnyenyekevu aliyetanguliza mbele uzalendo, uadilifu na uwajibikaji.
Aidha,ameshauri Watanzania wote kuzidi kuenzi falsafa zake na kuyaishi mema yote katika kumuenzi kwa vitendo.
Tags
Habari
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
Maliasili na Utalii
Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere
Michezo