NA HAPPINESS SHAYO-WMU
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kusimamia vyema maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro baina ya shughuli za kibinadamu na hifadhi.

“Kila mtu akisimamia eneo lake vizuri hii migogoro itapungua sana ama kuisha lakini tukisubiri Serikali iseme au Kamati ya Mawaziri iseme, maeneo ya hifadhi yatakwisha,” Mhe. Masanja amesisitiza.

Mhe. Masanja amewaelekeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Watendaji wa Vijiji kuhakiki wahamiaji wanaoingia katika maeneo yao ili kujua sababu inayowafanya waanzishe vijiji katika hifadhi na pia watoe maelekezo ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi na kuwasimamia ili kuondokana na migogoro ya ardhi.
“Ifike mahala wananchi wafahamu umuhimu wa uhifadhi na shughuli za kibinadamu” ameongeza.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameelekeza migogoro hiyo itatuliwe ambapo kwa sasa hifadhi zinaheshimika na wananchi wanaendelea na maisha yao ya kila siku.