NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kuendeleza viwanja vyake 60 vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini.
Uendelezaji huo unatarajiwa kuwa shirikishi baina ya shirika na sekta binafsi ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuzindua Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa, ambayo itafanyika Oktoba 21, 2022 jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Uendelezaji Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), William Genya ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Bw.Genya aliambatana na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Taifa la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Muungano Saguya, ambapo amesema uzinduzi huo utafanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JICC).
Genya amesema kuwa, hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa mahitaji ya nyumba na upungufu wa nyumba za wapangaji hivyo, shirika kupitia uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu itaingia ubia na sekta binafsi ili kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo.
Amesema, katika viwanja hivyo 60 ambavyo vipo katika maeneo ya kimkakati, 40 vinapatikana jijini Dar es Salaam na 20 vinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia amesema, ili kuongeza thamani ya nyumba zake na maeneo zilipo, shirika litabomoa nyumba ambazo zimeonekana kuchoka kwa ajili ya kujenga za kisasa.
“Kuna viwanja 60 vinavyotakiwa kujengwa nyumba za wapangaji kati ya hivyo 40 vipo Mkoa wa Dar es Salaam na 20 vipo mikoani ambavyo navyo vitajengwa nyumba za wapangaji. Mfano, kuna eneo la wazi ambalo linatumika kama Parking Posta nalo litatumika kwa ujenzi wa nyumba za wapangaji na biashara na viwanja vingine vipo mkoa ya Mwanza, Arusha lakini kabla ya kuanza miradi hiyo tutazungumza na wahusika ili kuweka mambo sawa,na baada ya mradi kukamilika watapewa kipaumbele cha kwanza,"amesema Mkurugenzi huyo.
Awali, Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Taifa la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Muungano Saguya amesema,uzinduzi huo ni moja ya wapo ya hatua ya mwendelezo wa utekelezaji wa vipaumbele 11 vya shirika ambavyo vinatekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2022/23 .
"Kama mnakumbuka mwezi Julai, mwaka huu tulielezea vipaumbele 11 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 moja ya kipaumbele ni kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya ubia kati yao na NHC.
"Leo nimewaita kuwaelezea kuhusu uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa. Sera ya ubia ambayo tunawaalika Watanzania kushiriki ilianzishwa na shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika. Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 na yamezingatia kuvutia uwekezaji kwa kuwa yana maslahi kwa shirika na mwekezaji na yameshapitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika.
"Kwa hiyo,shirika sasa linakwenda kuzindua Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa tarehe 21 mwezi huu wa Oktoba 2022, tunakwenda kuwa na tukio hilo muhimu kubwa linakwenda kuishirikisha sekta binafsi na wawekezaji kutoka ndani ya nchi ambao wamealikwa katika uzinduzi huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) kuanzia saa tatu asubuhi,"amesema Saguya.
"Uzinduzi wa sera hii iliyoboreshwa unalenga kuwa na maslahi mapana kwa shirika, wawekezaji na Taifa kwa ujumla, unalenga kuwapatia fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini,"amebainisha Bw.Saguya.
"Katika
uzinduzi huu mkubwa tunakusudia kuwa na washiriki takribani 600 kutoka
taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, vyama na bodi za kitaaluma
pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao
wamealikwa,"amefafanua Bw.Saguya.
Pia Bw.Saguya
amebainisha kuwa,mabalozi wa nchi zenye wawekezaji wakubwa wamealikwa
na wawakilishi wa Kamati za Bunge zinazogusa shughuli za shirika
wamealikwa pia.
"Kwa
mawasiliano zaidi juu ya kushiriki kwenye uzinduzi huo tafadhali piga
simu nambari +255 767 566 299 au +255 658 662 800 au tutumie ujumbe
kupitia baruapepe nhcjv@nhc.co.tz,"amesisitiza Bw.Saguya.