Nyumba ya DED Nkasi yateketea kwa moto asema 'nimebaki na nguo tu',mwaka juzi iliteketea ya DED Meatu

NA DIRAMAKINI

NYUMBA ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, William Mwakalambile imeteketea kwa moto wakati akiwa katika kikao cha kamati ya kudhibiti ukimwi ya halamsahauri hiyo na hivyo kushindwa kuokoa kitu chochote toka ndani ya nyumba hiyo.

"Kwa kweli moto ulikuwa ni mkubwa tulishindwa kuokoa kitu chochote kile na vitu vyangu vyote vimeteketea, hapa nilipo nimebaki na nguo nilizovaa mwilini tu, kwa kweli hii ni hasara kubwa;

Mkurugenzi huyo amesema kuwa, tukio hilo likitokea siku ya Oktoba 12,2022 majira ya saa 6:30 mchana wakati akiwa ofisini akiendelea na kikao.

Amesema kuwa, akiwa anaendelea na kikao alipigiwa simu na kuambiwa kuwa nyumba yake inawaka moto ambapo alilazimika kuondoka kwenye kikao hicho na kurudi nyumbani kusaidiana na majirani kuuzima moto huo.

Mwakalambile amesema, alipofika alikuta moto huo umeshika kasi kiasi kwamba ilishindikana kuuzima kutokana na kutokuwa na vifaa vya kuzimia moto badala yake walikaa wakisubiri gari la zimamoto likiwa linatokea mjini Sumbawanga ili likafanye kazi ya kuzima moto.

Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoani Rukwa, Gervas Fungamali akizungumzia tukukio hilo amesema kuwa, gari la zimamoto lilifanikiwa kufika eneo la tukio, lakini kutokana na umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka mjini Sumbawanga lilopo gari hilo hadi wilayani Nkasi walikuta sehemu kubwa ya nyumba hiyo imeteketea.

Amesema kuwa, askari wa zimamoto walijitahidi kuuzima moto huo na kufanikiwa kuokoa vitu vichache lakini sehemu kubwa ya mali iliyokuwemo kwenye nyumba hiyo iliteketea.

Pia amesema kuwa,nyumba hiyo ilikuwa haina kifaa chochote cha kuzimia moto wala vifaa vya kutoa taarifa kama kuna chanzo cha moto, hivyo hata wananchi waliofika kutoa msaada walifika kwa kuchelewa na kukuta moto umewaka sehemu kubwa ya nyumba hiyo.

Kamanda huyo alisema kuwa uchunguzi wa awali inadhaniwa kuwa chanzo cha moto huo ni kutokana na hitilafu ya umeme, kwani moto huo unaonesha ulianzia kwenye chumba alichokua analala Mkurugenzi huyo, lakini uchunguzi bado unaendelea.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Wenceslaus Kapita amesema kuwa, halamsahauri hiyo imempa hifadhi Mkurugenzi huyo katika eneo jingine wakati wakisubiri utaratibu mwingine wa serikali ukiendelea.

MWAKA 2020

Ikumbukwe kuwa, Novemba 14, 2020 nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu nayo iliteketea kwa moto kama picha inavyoonekana hapa chini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news