NA HAPPINESS SHAYO-WMU
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) amesema, uwepo Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili (S!TE) katika Jiji la Dar es Salaam ni fursa kubwa kwa jiji hilo kutangaza vivutio vyake.
Amesema kuwa, Jiji la Dar es Salaam ndio lango Kuu la Biashara Tanzania na kwamba wageni wengi wanaofika nchini wanafikia katika Jiji hilo na kisha kuelekea kwenye maeneo mengine ya utalii.
Mhe.Masanja ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Oktoba 21,2022 wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam linapofanyika Onesho la S!TE 2022.
Aidha, ameeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam lina historia ya kipekee kutokana na vivutio vilivyopo vya kiutamaduni ikiwemo majengo na malikale.
“Jiji la Dar es Salaam lina historia kubwa na nzuri ya kiutalii kutokana na uasilia wake. Kuna maeneo mengi ya kiutalii ikiwemo majengo na malikale hivyo Onesho hili litafungua fursa za kiutalii katika Jiji hili,”amesema Mhe. Masanja.