PICHA HIYO INASEMA:Apewe zake heshima

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tangu mwezi Juni, mwaka huu imeendelea kutoa ruzuku ya mafuta ambayo ilianza na shilingi bilioni 100 kwa mwezi.

Mheshimiwa Rais Samia aliagiza ruzuku hiyo itolewe kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida ya Serikali (recurrent expenditure) kila mwezi kuanzia Juni, mwaka huu hadi hapo bei za mafuta katika soko la Dunia zitulie.

Bei za mafuta katika soko la Dunia ziliongezeka zaidi kutokana na pamoja na mambo mengine, vita kati ya Urusi na Ukraine ambayo ilianza mwishoni mwa mwezi Februari, mwaka huu.

Vita hiyo ilisababisha kuharibika kwa mfumo wa usambazaji wa mafuta kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi, hivyo kuongezeka kwa bei za mafuta ghafi duniani.

Hata hivyo, maamuzi magumu na ya kishujaa ya Serikali katika kujibana kwenye matumizi yake ili ipatikane ruzuku hiyo yamesababisha bei za mafuta nchini ziteremke kwa asilimia kubwa kuanzia Juni Mosi, mwaka huu hadi Oktoba, mwaka huu ambapo pia Serikali imetoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 59.58.

Lengo likiwa ni kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei ya mafuta hapa nchini kwa wananchi na uchumi kwa ujumla. Ungana na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande hapa chini uweze kujifunza jambo kupitia haya;

1.Mstahili heshima,
Apewe yake heshima,
Wa kubebeshwa lawama,
Hizo ni saizi yake.

2.Rais wetu ni mama,
Apewe zake heshima,
Afanya tunajinoma,
Kwa hii mipango yake.

3.Niyajuayo nasema,
Niyaonayo mazima,
Nishati hii nasema,
Kongole kwake zifike.

4.Msije mkanisema,
Kwamba ninasemasema,
Picha hiyo inasema,
Yule mwenye macho yake.

5.Tanzania yasimama,
Sababu ya kujituma,
Tumepunguziwa homa,
Mafuta makali yake.

6. Bei zinavyozizima,
Hata bajeti kukwama,
Sisi vema zasimama,
Haya maamuzi yake.

7.Ruzuku ile nasema,
Mabilioni kutema,
Yanapunguza noma,
Hongera zifike kwake.

8.Kifua mbele kusema,
Nafuu ya kwetu nzima,
Kwa kweli ni jambo jema,
Kongole mipango yake.

9.EWURA tumemsoma,
Juzi vile amesema,
Bei zilizosimama,
Twaona nafuu yake.

10. Elfu kumi nasema,
Lita tatu ziligoma,
Sasa ni nini twasema,
Hongera kote zifike.

11.Bei zinapoyoyoma,
Hata kuzidi kuuma,
Hakuna pa kusimama,
Bei zingine zinyoke.

12.Zinaposhuka salama,
Zinagusa nchi nzima,
Bei zote zasimama,
Hebu tuache tucheke.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news