NA DIRAMAKINI
VITIVO vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania vimetakiwa kubuni mitaala inayotoa taaluma zitazokuwa ni msaada kwa mabadiliko ya kiuchumi kwa wahitimu na nchi kwa ujumla badala ya kuendelea kufikiria programu ambazo hazimpatii mhitimu ujuzi unaomuwezesha kuleta mabadiliko yake kiuchumi na taifa kwa jumla.
Wito huu umetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Elifas Bisanda, wakati wa mkutano na watumishi wote ulioitishwa Oktoba 11, 2022, Makao Makuu ya chuo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Licha ya kwamba tunataka mitaala inayoendana na matakwa ya mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) ili kukidhi haja za mradi huo lakini lengo letu ni kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa jamii. Tuwe na programu ambazo mtu akifundishwa hatoki kwenda kutafuta kazi.”
Hali kadhalika, Prof. Bisanda, aliwasisitiza watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutoa huduma bora kwa wanafunzi na wateja wote wanaofika katika ofisi za chuo kupata huduma mbalimbali.
Amewataka watumishi kuonesha utofauti wa huduma kwa kuwajali na kuonesha ukarimu kwa wanafunzi na wateja wote wa chuo ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi hata mmoja anapotea kwa kukosa huduma nzuri.
"Chuo chetu kina utofauti na vyuo vingine hasa vile vya bweni kwa sababu wanafunzi wetu hawakai sehemu moja na hivyo kila mmoja anaweza kuja kwa wakati wake kutaka huduma. Pia, mfumo wetu wa ufundishaji ni tofauti na vyuo vingine na pia ni tofauti na kule wanafunzi walipotoka. Hivyo wanakuwa na mambo mengi ambayo wanataka kufahamu. Tujitahidi kuwapatia maelekezo kwa ukarimu na upendo kwa kila wanachouliza,"alisema Prof. Bisanda.
Pia, katika kikao hicho naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania - Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam Prof. Deus Ngaruko, amesema mradi wa HEET umeletwa kwa malengo ya kugusa moja kwa moja kwenye mitaala iliyojikita katika ujuzi, ambapo mitaala hiyo inatakiwa kuzalisha wataalam na wajuzi wenye ubobezi wa kuzalisha ajira na huduma zenye tija kwa taifa.
"Niwarai wativa na wakurugenzi kuhakikisha tunaanzisha programu ambazo zitasaidia kutoa wahitimu ambao wataweza kujiajiri tangu wakiwa katika masomo na wanapohitimu wanaendeleza ajira hizo kwa vijana wengine katika jamii. Kila mmoja wetu aende akafikiri, asome, apate uzoefu kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili tuje na programu mujarabu za kutoa wahitimu mahiri na wenye ujuzi wa kutosha,"alisema Prof.Ngaruko.
Aidha Prof. George Oreku ambaye ni naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango amewataka watumishi kuwa na utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuondoa usumbufu wa ufuatiliaji wa mafao pindi mtumishi anapostaafu utumishi wa umma.
Prof.Oreku amesisitiza kuwa, kila mtumishi hana budi kutembelea akaunti yake inayopatikana kwa urahisi mtandaoni ili kuona mwenendo wa michango yake na atakapobaini mapengo atoe taarifa ili yafanyiwe kazi kwa wakati.
"Ndugu wafanyakazi, natoa rai kwenu nyote kwamba tujenge utamaduni wa kutembelea akaunti zetu za mifuko ya hifadhi ya jamii mara kwa mara ili kujionea maendeleo ya michango yetu. Siku hizi mambo ni rahisi mno wala huitaji kwenda kwenye ofisi za mfuko husika bali hapo hapo kiganjani kwako unaweza kuingia kwenye akaunti yako na ukapata taarifa za michango yako yote,"alibainisha Prof. Oreku.
Kwa upande wake naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma na Mikoa Prof.Alex Makulilo, amewapongeza wakurugenzi wa vituo vya mikoa kwa namna wanavyojituma katika kufanya kazi na kutimiza majukumu yao ya kila siku.
"Nawakumbusha wafanyakazi wote wa vituo vya mikoa vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wakuu wa vituo, kurugenzi na idara ili kuleta ufanisi katika vituo vyao. Sambamba na hilo, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ni wajibu kwa kila mtumishi. Tufanye kazi kwa weledi na maarifa katika kuwahudumia wanafunzi wetu,"alisema Prof. Makulilo.