NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo kwa kushirikiana na Vi Agroforestry wanatarajia kugawa bure miche ya miti na matunda ipatayo 100,000 kwa taasisi mbalimbali zikiwemo shule, zahanati na kwa wanavijiji ndani ya jimbo hilo.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 25, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini. Ambapo taarifa hoyo imeeleza kuwa miche hiyo itagawiwa wakati wa mvua za vuli mwezi Novemba hadi Desemba, 2022 ikihusisha miche ya matunda, mbao, kuni, madawa ya asili pamoja na ufugaji wa nyuki.
Mheshimiwa Prof. Muhongo, amekuwa akishirikiana na VI Agroforestry ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Sweden na imekuwa ikifanya vizuri katika utunzaji wa mazingira ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini na maeneo mengine mkoani Mara.
Ambapo mpaka sasa matayarisho ya miche 100,000 chini ya mtaalamu Jacob Malima yanaendelea vizuri ndani ya kitalu cha VI Agroforestry kilichopo Manispaa ya Musoma.
Aidha, taarifa hiyo ya Jimbo la Musoma Vijijini imetoa ombi kwa serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
"Jimbo la Musoma Vijijini linaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii ifufue kitalu cha miti cha Serikali kilichopo Kijijini Suguti," imeeleza Sehemu ya taarifa hiyo.
Juu ni pichani zinamuonyesha Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo akiwa kwenye Kitalu cha VI Agroforestry kinachotayarisha miche 100,000 ya miti na matunda.