NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kudumisha dhamira ya kweli katika kutafuta maelewano ya kisiasa na kijamii hapa nchini, ili kujenga mustakabali mwema wa Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Kujadili Masuala Mahsusi ya Zanzibar Yanayohu Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa na kulia kwa Rais ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mstaafu Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Mhe. Jaji Francis Mutungi. (Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kujadili masuala mahususi ya Zanzibar yanayohusu Dsemokrasia ya Vyama vya Siasa, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport Zanzibar.
Amesema, Zanzibar haiwezi kufikia maelewano ya kweli ya kisiasa, ikiwa jamii badala ya kushirikiana kurekebisha kasoro zinazojitokeza, baadhi ya watu wanatafuta visingizo vya kulaumiana.
Amesema ili kufikia hatua ya maelewano, kuna umuhimu mkubwa wa kuvumiliana, kustahamiliana pamoja na kusahau mambo mbali yaliopita.
“Maelewano ya kijamii hayawezi kudumu iwapo kila siku mtakuwa mnakumbushana au kutishana kwa mambo yaliopita,”amesema.
Ameeleza kuwa, kiini cha maridhiano ni ujasiri na kuachana na mambo yaliopita na kusema maelewano hayawezi kudumu iwapo wahusika watakuwa hawaaminiani.
Aidha, amebainisha mambo mbalimbali ambayo jamii inapaswa kuyazingatia ili kufikia maelewano ya kweli, ikiwemo kukubaliana juu ya mgawanyo wa majukumu ya ndani ya maelewamo au maridhiano yaliofikiwa.
Amesema, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika iliyo na utulivu mkubwa wa kisiasa na yenye utamaduni wa kuvumiliana na hivyo akasisitiza haja ya kuendeleza utamaduni huo.
Aidha, Dkt.Mwinyi amewataka viongozi na wadau wa siasa kutoruhusu itikadi zao za kisiasa kudhoofisha undugu, umoja na mshikamano uliopo, na kubainisha umuhimu wa kukaa pamoja ili kufikia suluhisho la kuondokana na tofauti za kisiasa.
“Tukae na kuzungumza ili kuondoa tofauti zetu ili tubakike wamoja, tudumishe amani na utulivu ii kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,”amesema.
Amesema,viongozi wa kisiasa pamoja na wadau wa siasa wana wajibu wa kukubaliana na uwepo wa tofauti za kisiasa baina yao na kwamwe wasiruhusu hali hiyo kuwa chanzo cha kufarikiana na kuhasimiana.
Vile vile aliwataka wadau wa siasa kuondokana na utaratibu utakaowajengea mazingira wanasiasa kubadilika na badala yake wawawekee mazingira bora ya kimaendeleo pamoja na kudumisha upendo na umoja wa kitaifa.
Katika hatua nyingine, aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia hekima, busara na uzoefu wao katika kutoa, kuchangia na kutetea hoja zinazowasilishwa ili hatimae waweze kupata mapendekezo na maazimio yalio bora.
Dkt.Mwinyi alibainisha matarajio yake kuwa mjadala huo utatekelezwa na kuhakikisha nchi inafanya siasa za kistaarabu ili kujenga misingi ya amani na utulivu.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote waliochangia kufanikisha mkutano huo, ikiwemo washirika wa maendeleo wa UNDP, NDI, IRI pamoja na USAID.
Naye Waziri wa Nchi (OMPR) Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia vyema fursa waliyoipata, akibainisha kuwa ni muhimu na adhimu, kwa kigezo kuwa kuna baadhi nchi wanaihitaji na hawaipati.
Aidha, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi alisema mkutano huo umewahusisha washirki kutoka katika makundi mbali mbali, ikiwemo Viongozi wa Vyama 19 vya Siasa, Mawaziri, Makatibu wakuu, Asasi za Kiraia, watu mashuhuri, Viongozi wa Dini pamoja na wanasiasa.
Alisema katika mkutano huo jumla ya mada nne zitawasilishwa, ikiwemo ya Masuala mahsusi ya Zanzibar yanayohusus Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa Zanzibar.
Mapema, Mwenyekiti wa Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu alisema kufanyika kwa mkutano huo ni jambo kubwa lenye mnasaba na misingi ya Utawala Bora, huku akimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuasisi mkutano huo wa kihistoria.
Pia amewataka wajumbe wa mkutano huo kuelezea mambo muhimu ya msingi wa kitaifa kwa kuweka mbele uzalendo.