Rais Dkt.Mwinyi:Kilimo, viwanda ni sekta muhimu sana

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuhamasisha kilimo pamoja na kuunga mkono Sekta ya Viwanda kwa kutambua kuwa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa pili kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wachakata nafaka (IAOM MEA 2022), Bw.Mounir Bakhresa (kulia),pamoja na Viongozi wengiune akiwepo Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe.Omar Said Shaabani (katikati) kabla ya kuufungua Oktoba 26, 2022 katika Hoteli ya Verde Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo alipozungumza na washiriki wa Mkutano wa 32 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wachakataji Nafaka (IAOM) uliofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni, Mkoa Mjini Magharibi.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya kila juhudi kuhakikisha inaimarishaji uzalishaji wa mazao ya kilimo, ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ina mchango muhimu katika kuwahakikishia wananchi usalama wa chakula.
Ameeleza kuwa, mazao ya kilimo yana umuhimu mkubwa katika uimarishaji na uendelezaji wa viwanda kwani mazao hayo ndio yanayotumika kama rasilimali za viwandani.

Dkt.Mwinyi amesema Dunia inakabiliwa na changamaoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri uzalishaji wa chakula, wakati huu dunia ikipita katika wakati mgumu kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Amesema nchi za Urusi na Ukraine ndio wasambaji wakubwa wa mazao ya mafuta, zao la ngano pamoja na mbolea, hivyo vita vinavyoendelea vinaathiri mnyonyoro wa usambazaji wa chakula katika maeneo mbalimbali duniani, huku hali hiyo ikichangia upandaji wa bei ya mbolea.
Dkt.Mwinyi amesema mkutano huo umekuja kwa wakati muafaka kwa kuamini kuwa huenda ukasaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya chakula nchini.

Amewataka wajumbe kujadili pamoja na kuja na mipango itakayobainisha namna ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza gharama pamoja na kuongeza uhifadhi wa chakula, sambamba na kuimarisha teknolojia katika sekta hiyo.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwataka wajumbe kuangalia fursa mbalimbali katika sekta zinazopatikana Zanzibar na kuja kuwekeza.

Amesema Zanzibar inatafuta wawekezaji walio tayari kufanya kazi na Serikali katika utekelezaji wa sera yake ya Uchumi wa Buluu, inayohusisha masuala ya uvuvi, mafuta na gesi, utalii pamoja na usafiri wa majini.
Naye, Waziri wa Biashara, Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaaban amesema kuwa mkutano huo umekuja wakati mwafaka, wakati ambapo serikali imejikita katika kutenegeneza fursa na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Mapema, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bakhresa Grain Milling,Mounir Bakhresa aliishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa inayotoa, huku akibainisha faida kubwa itakayopatikana kwa vile mkutano huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya Serikali, wakati huu Dunia ikakabiliwa na changamoto kubwaya chakula.

Mkutano wa 32 wa mwaka ‘MIDEAST AND AFRIKA CONFRENCE AND EXPO IAOM, umehudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wasambazaji wa vyakula, ambapo unajadili hali ya mdororo wa uzalishaji wa chakula pamoja na changamoto zinazojitokeza duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news