NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza uhusiano na ushirikiano baina yao kwa kuzingatia udugu wa kihistoria uliopo.
PICHA NA IKULU.
Dkt. Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Fred Mwesigye, aliyefika kujitambulisha.
Amesema, wananchi wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki wana udugu wa kihistoria, hivyo ni vyema kuwepo utaratibu wa kutembeleana na kushirikiana katika mambo mbalimbali.
Ameeleza kuwa, Zanzibar ni kisiwa ambapo Sekta ya Utalii imepewa kipaumbele na kusema kuna maeneo mbalimbali ya kushirikiana.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kibiashara kati ya Uganda na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa viongozi kufanya mazungumzo ili kuwawezesha wafanyabaishara wa nchi mbili hizo kuendeleza biashara zao.
Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Museveni kwa mwaliko aliotuma kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan wa kuzuru nchi hiyo hapo baadae, ambapo Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kumwakilisha.
“Naomba unifikishie salamu zangu za dhati kwa Rais Museveni...tunafahamiana kwa kipindi kirefu sasa,”amesema.
Naye, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Fred Mwesigye amesema nchi hiyo inahitaji walimu wa kufundisha Lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar baada ya Serikali kufikia uamuzi wa kuanzisha somo la Lugha ya Kiswahili katika mitaala ya shule zote nchini humo.
Amesema, kupitia wadhifa wake wa Ubalozi, atatumia nafasi hiyo kuutangaza uzuri wa Zanzibar nchini humo, ikiwa hatua ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo.
Aidha, amesema Uganda inathamini mchango mkubwa wa wananchi wa Serikali ya Tanzania, hususani katika suala la Ukombozi wa Bara za Afrika pamoja na kuisaidia Uganda katika harakati za kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Dikteta Idd Amin Dada mnamo mwaka 1978.