NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia wananchi wa Kitongoji cha Ikanka kilichopo Kijiji cha Itumba Wilaya ya Ileje kuendelea kuishi sehemu ya eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range mkoani Songwe.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifurahi na wananchi wa kitongoji cha Ikanka katika kijiji Itumba wilayani Ileje wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea kitongoji hicho jana.
Uamuzi huo unakifanya Kitongoji cha Nkanka sasa kutambuliwa ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range kutokana na idadi ya kaya 105 zenye makazi zilizopo ndani ya eneo.
Aidha, uamuzi huo pia umegusia mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi za msitu wa Mugombezi uliopo Kijiji cha Nyimbili katika Kata ya Mlowo, Ilengo Mbozi mkoani Songwe.
Akitangaza uamuzi huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt.Angeline Mabula amesema sehemu ya eneo la hifadhi ekari 278 zitamegwa na kubaki kwa wananchi kutoka ekari 414 kwa kuwa eneo hilo limeendelezwa kwa shighuli za kilimo, makazi na kuwekwa huduma za kijamii kama uwanja wa mpira na pampu ya maji.
Waziri Mabula amewatahadharisha wananchi walioruhusiwa kuendelea eneo hilo kutojaribu kuongeza maeneo wanayoishi huku akieleleza kuwa, mara baada ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kukamilika maeneo yote ya hifadhi yanatakiwa kulindwa.
Aidha, Dkt.Mabula ambaye alikuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikanka Oktoba 24, 2022 akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta aliagiza shughuli za kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji nazo zisitishwe ili kunusuru vyanzo vya maji ndani ya hifadhi.
Naibu Waziri wa Kilimo Athony Mavunde,akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kitongoji cha Ikanka Ileje Songwe.
Kwa upande wao Mawaziri walioambatana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi walisisitiza umuhimu wa kutunzwa mazingira pamoja na kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa maeneo yote yaliyomegwa.
Naibu waziri wa Maji, Meryprisca Mahundi aliwaambia wananchi wa Kitongoji cha Ikanka kuwa, baada ya kuruhusiwa kuendelea kuishi eneo hilo wahakikishe wanatunza na kuhifadhi vyanzo vya maji na kuepuka shughuli zozote zitakazosababisha uharibifu wa vyanzo hivyo.
Khamis Hamza Chilo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira alisisitiza suala la wananchi kupanda miti katika maeneo waliyoachiwa ili kutunza mazingira.
Naibu Waziri wa Kilimo Athony Mavunde,akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kitongoji cha Ikanka Ileje Songwe.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde pamoja na Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi , Abdallah Ulega walieleza umuhimu wa maeneo yaliyomegwa kupangiwa matumizi ya ardhi na kupimwa sambamba na kuanishwaa maeneo ya kilimo, mifugo pamoja na uvuvi ili kuepuka kutengeneza migogoro mingine.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akizungumza katika mkutano na wananchi wa Ikanka Ileje Songwe jana.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amewataka viongozi wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatekeleza maamuzi ya baraza la mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kwa kuweka mpango wa utekelezaji hasa kwa yale maeneo ambayo hayana tathmini ya kina.
Katika maamuzi yake, Baraza la Mawaziri liliamua vijiji 920 kati ya 975 vyenye migogoro katika ranchi, mapori ya akiba, mashamba na vyanzo vya maji kubaki ingawa baadhi ya vijiji vitahusisha marekebisho ya mipaka kwa njia shirikishi,
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Ikanka katika Kijiji Itumba wilayani Ileje wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea kitongoji hicho.(Picha na WANMM).
Hata hivyo, vijiji 55 kati ya 975 vinaendelea kufanyiwa tathmini na kamati na wataalamu wake kutoa mapendekezo kwa ajili ya maamuzi.
Tayari kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta imeshatembelea mikoa kumi na tisa kati 26 kamati imeshapeleka mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri na inaendelea na ziara yake kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.