NA STEVEN NYAMITI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuendelea kufanya vizuri katika kuisimamia Sekta hiyo hapa nchini ili iwe chachu ya kitovu cha uchumi.

Aidha, amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa wananchi wa mkoa wa Geita katika ujenzi wa uchumi hususan kwa kupitia shughuli za uchimbaji wa madini.

Mara baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha dhahabu, Rais Samia amewataka wanachi wa Geita na mikoa yote inayochimba madini ya dhahabu kuvitumia viwanda vya kisasa vya kusafisha na kuchenjua dhahabu vilivyopo nchini mara baada ya kuzindua kiwanda cha Mama Masasi cha Geita.
"Niombe sana tupeleke dhahabu zetu huko zikachenjuliwe ili Tanzania iongeze thamani ya madini ya dhahabu yenye thamani kubwa," amesisitiza.

Vile vile, Rais ameitaka wizara kuendelea kutoa elimu juu ya Sheria ya Madini na Kanuni zake kwa wadau mbalimbali kupitia mafunzo maalum.
Rais Samia ameitaka Wizara ya Madini kuendelea kushirikiana na idara nyingine za Serikali na vyombo vya Dola mkoani na katika sehemu nyingine ambayo kuna uchimbaji mkubwa katika kusimamia shughuli za uzalishaji na biashara ya madini na kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini.

Kuhusu suala la kodi kwa wachimbaji ameiagiza Wizara ya Madini kukutana na Wizara ya Fedha kuziangalia na kuwasikiliza wadau na wafanyabiashara kuhusu kodi zinazoleta kero na kupunguza kasi ya utendaji kwa wawekezaji wanaowekeza katika Sekta hiyo.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema, mkoa wa Geita ni mkoa kinara wa dhahabu nchini. Ameongeza Geita ni ya kwanza katika mikoa inayozalisha dhahabu hapa Tanzania.
Dkt. Biteko amemhakikishia Rais Samia kuwa Sekta ya Madini itafikia lengo la makusanyo iliyopangiwa kupitia miradi mbalimbali ya uchimbaji madini inayoendela sasa katika maeneo mbalimbali.