Rais Samia atoa salamu za pole kifo cha Mbunge Mussa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kutokana na kifo cha Mbunge wa Jimbo la Amani visiwani Zanzibar,Mheshimiwa Mussa Hassan Mussa.

Mheshimiwa Rais Samia ametoa salamu hizo za pole leo Oktoba 13, 2022 ikiwa ni saa chache zimepita tangu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson kutoa taarifa ya kifo hicho.

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe.Mussa Hassan Mussa, Mbunge wa Jimbo la Amani (CCM), Zanzibar. Natuma salamu za pole kwa Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, familia na wakaazi wa Jimbo la Amani. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema Peponi, Amina,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Awali kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson imeeleza kuwa, Mheshimiwa Mussa Hassan Mussa amefariki leo akiwa nyumbani jijini Zanzibar.

Aidha, Mheshimiwa Spika ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wabunge pamoja na wananchi wa jimbo la Amani kufuatia msiba huo.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mhe.Mussa Hassan Mussa, natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, waheshimiwa wabunge na wananchi wa Jimbo la Amani.

"Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa Spika wa Bunge, Dkt.Tulia Ackson ametangaza kifo hicho.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia, mwili wa marehemu umepelekwa kijijini kwao Bwejuu kwa ajili ya maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news