RISASI HATANDIKWI KILA MTU

NA ADELADIUS MAKWEGA

ENEO la Mbagala Sabasaba-Mbuyuni jijini Dar es Salaam, tangu enzi lilikuwa na koo mbili za Kipogoro akina Makwega na akina Kazingoma, koo hizi mbili zote zinatokea kijiji kimoja na kata moja huko wilayani Ulanga, mkoani Morogoro.
Kazingoma mwenyewe sasa ni marehemu, kwa asili mzee huyu alikuwa akifanya kazi mbalimbali za mikono, lakini pia akifanya kazi moja kubwa sana kwa wakristo wa eneo hili ya kuziosha maiti zao kabla ya maziko.

Nyumbani kwake ni sehemu maaarufu mno kwa uuzwaji wa pombe za kienyeji tangu miaka ya 1950 hadi leo hii na kazi hiyo imekuwa ikirithishiwa kutoka kwa kizazi kimoja kwenda kingine. Mara zote nyumba yao haikosi wageni iwe barazani, ndani ya vyumba au uani, kona zote huwa zimejaa wateja.

Nyumba hii kwa kuwa ipo jirani na kwetu kila ninapofika Dar es Salaam ninawajibu wa kufika hapo na kuwasalimu kwa heshima zote ndugu zangu.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikijiuliza jambo moja linalonishangaza mno japokuwa tupo nao jirani akina Kazingoma lakini koo hizi mbili hazijaoleana iwe kwa siri au wazi, hilo linanipa picha kuwa hawa ndugu wakubwa sana tangu enzi.

Kila wao au sisi linapotokea tatizo la kifamilia vikaoni tunakuwa pamoja tukishirikiana namna ya kulitatua.

Kwa majuma kadhaa sasa nipo Dar es Salaam, nilifika nyumbani kwa Kazingoma kama ada yangu na kukaribishwa katika dawati maalumu na kuwasabai. 

Nilitumia zaidi ya dakika 45 kuongea na ndugu zangu hawa. Madhari ya Nyumbani kwa Kazingoma ilikuwa ya wateja wengi nje na ndani ya makazi haya, jua kali liliwaka huku wateja wao na mie ndugu yao tukibariza chini ya mti uliokuwa na kivuli kizuri mno.“Naona hapa pana hewa inayotoka katika kivuli cha mti huu, Je huu ni Mkungu?”.
Walinicheka sana, kijana mmoja akasema, “Makwega kwa umri wako unapaswa kuifahamu miti yote vizuri sana kwa majina na kazi zake, ili utuambiwe wadogo zako kama huu ni dawa au siyo. Inawezekana wadogo zako tukazunguka huko na kule tukapata shida, tukija kwako, unatuambia chimbeni mti huu na huo, tunapata dawa tunapona. Sasa wewe hata mti huu ulio usoni kwako hautambui, je tutakuwa salama?”.

Mwanakwetu nilisalimu amri kwa hoja hiyo, nikajibu mtakuwa salama tu ”Huu ni MTOMONDO na majani yake yanafanana fika na ya Mkungu.Unauona kila siku lakini leo Mungu amekupa bahati uulize ili uufahamu.”

Ndugu zangu hawa waliendelea kuuza pombe yao ya kienyeji, nikaulizwa, Umeshawai kusikia jina la Kijiji cha KITOMONDO? Nikajibu ndiyo nafahamu kidogo, ukiwa unakwenda Kisiju Pwani, ukitokea pale Mkuranga kuna kijiji kinatwa Kitomondo na jina hilo linatokana na mti huu, nilielekezwa.
"Mtomondo unamea sana katika vyanzo vya maji, lakini ni jambo la kushangaza mno mbona hapa umestawi hapa mbali na vyanzo vya maji? Kwa simulizi za Mzee Kazingoma mwenyewe alidai kuwa eneo hili lilikuwa na choo cha shimo, hivyo Mtomondo mmojawapo ulikuwa ni miongoni mwa magogo yaliyotumika kujengea, maji ya kuoga pahala hapa yaliustawisha na hadi leo umekuwa mti mkubwa, kama unavyouona, tunavyopata hisani ya kivuli chake.”

Ipo miti kadhaa ya Tanzania yenye tabia hiyo mathalani Mjenga Ua inaweza kuota kama huu. Niliendelea kupata darasa la mti huu,“Kivuli chake kinawasaidia mno viumbe wa eneo ulipoota katika maji kujipumzisha na kuzuia kupigwa na jua moja kwa moja.Nayo majani yake yakiwa kama maboya yanayoeleaelea.”

Kizuri hakikosi kasoro, "Ukiyachukua majani au magome yake ukayafikicha au kuyatwanga huwa yna madhara kwa viumbe walipo katika maji, baada ya muda machache viumbe kadhaa waliopo humu wataanza kuelea juu wakiwa wamelewa.Lakini yakianguka katika maji majani au magome yake hayana shida yoyote ile.”

Nikajiuliza sasa kwanini mti huu wenye madhara haya unastawi jirani na vyanzo vya maji?.

“Unapokabidhiwa bunduki siyo kwamba kila aliye jirani yako unamtandika risasi, ukifanya hivyo tutakupokonya bunduki hiyo na kukuadhibu.” Waliniambia ndugu hawa.

Pengine Mtomondo umepewa madhara unapofikichwa ili usiliwe na viumbe vinavyoweza kufika eneo hilo na ubaki kuwa salama wakati wote na kulinda mazingira ya maji hayo na viumbe hai wanaoishi.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news