SENSA WATU NA MAKAZI: NI MUDA WA MATOKEO

NA LWAGA MWAMBANDE

MWEZI Agosti, mwaka huu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Sensa ya Watu na Makazi. Zoezi ambalo lilifanikiwa kikamilifu ambapo Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) ilifanikisha maandalizi hayo.
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo, Sensa ya mwaka 2022 ilikuwa ni Sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.Baada ya Agosti, mwaka huu kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, leo Oktoba 31, 2022 ni wakati wetu wa kuyasubiria matokeo ya zoezi hilo muhimu, matokeo ambayo yatatolewa saa chache zijazo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, endelea;

1:Mama katukaribisha, Uwanja wa Jamhuri,
Ujumbe kaufikisha, umesomeka vizuri,
Na sisi twaliamsha, tukashiriki vizuri,
Uzinduzi matokeo, Sensa watu na makazi.

2:Dodoma twaliamsha, siku tuloisubiri,
Tulivyojishirikisha, kuhesabika vizuri,
Sasa tunalianzisha, uchakataji mzuri,
Uzinduzi matokeo, Sensa watu na makazi.

3:Idadi tumefikisha, pamoja wetu umri,
Ndiyo wanawasilisha, tuweze pata habari,
Oktoba inaisha, na matokeo mazuri,
Uzinduzi matokeo, Sensa Watu na Makazi.

4:Rais litukumbusha, kujandikisha vizuri,
Na sisi hatukubisha, kutoa zetu habari,
Sasa tunakamilisha, zoezi la sense nzuri,
Uzinduzi matokeo, Sensa Watu na Makazi.

5:Alosema twakumbusha, kwanini sensa ni nzuri,
Matokeo tawezesha, mipangilio mizuri,
Miradi kuifikisha, kwa mgawanyo mzuri,
Uzinduzi matokeo, Sensa Watu na Makazi.

6:Rais kakaribisha, twende kule Jamhuri,
Uwanja kuushibisha, kungoja habari nzuri,
Ambazo tatuwezesha, kuwa mipango mizuri,
Sensa Watu na Makazi, ni muda wa matokeo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news