SERENGETI GIRLS: WAMEPIGA MTU HUKO!

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 15, 2022 imekuwa siku ya furaha na tabasamu kwa Watanzania, baada ya wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya miaka 17 huko India,Serengeti Girls kuwachapa Les Bleues ya Ufaransa mabao 2-1.

Mchezo huo wa kuvutia na wa aina yake umepigwa katika dimba la Fatorda (Pandit Jawaharlal Nehru) lilopo Margao, Goa nchini India.
Mabao ya Serengeti Girls yalifungwa na Diana Mnally dakika ya 16 na Christer Bahera dakika ya 56 kwa penalti, wakati la Ufaransa lilifungwa na Lucie Calba dakika ya 75. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hii ni ishara njema kwa Tanzania katika kuleta ushindani kupitia soka la Kimataifa, endelea hapa chini ujifunze;

1:Ni kwa mara ya kwanza, tangu kuumbwa dunia,
Wasichana wameanza, kung’arisha Tanzania,
Ufaransa mewafunza, nini Kombe la Dunia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

2:Kuteleza kuanguka, tofauti nakwambia,
Wasichana meinuka, huko watupambania,
Huko hasa kimenuka, adabu wamewatia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

3:Ushindi wa wasichana, huko kombe la dunia,
Tumefurahia sana, tena tunashangilia,
Hasa sasa tunaona, ushindi wamepania,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

4:Chini ya kumi na saba, wachezaji Tanzania,
Mabinti nchi wabeba, wanavyotushindania,
Mipira wanavyokaba, Ufaransa wanalia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

5:Huyo Diana Mnaly, goli la kwanza katia,
Christer na yeye goli, ushindi umetimia,
Kale kamoja kagoli, chali hao wanalia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

6:Wasichana waonesha, tunatisha Tanzania,
Nao huko wauwasha, moto bila kuzimia,
Wengine watakomesha, mechi watapoingia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

7:Heri tunawatakia, ipaishe Tanzania,
Uwanjani kuingia, bendera kushikilia,
Pazuri mtafikia, bila hata kuzimia,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

8:Hongera kwa wachezaji, timu yetu Tanzania,
Hongera wafundishaji, mbinu mnazotumia,
Asante kwa mahitaji, Serikali Tanzania,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

9:Juzi Tembo Warriors, makubwa lifutanyia,
Ni Serengeti Girls, makubwa watufanyia,
Tunafurahi kichizi, sifa zaja Tanzania,
Ni Serengeti Girls, wamepiga mtu huko.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news