NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
SERIKALI imeruhusu vijiji 46 katika mkoa wa Simiyu vilivyokuwa katika mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi kuendelea na shughuli za kibinadamu ambazo hazitaathiri shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na ndani ya eneo kinga la mita 500.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula (kushoto) akizungumza na Mawaziri wenzake wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta walipowasili mkoani Simiyu Oktoba 17, 2022. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
Aidha, vijiji viwili kati ya 48 vya Mkoa wa Simiyu vilivyokuwa katika mgogoro wa aina hiyo vinafanyiwa tathmini ili kumega eneo ndani ya hifadhi ya Jumuiya ya Jamii (WMA).
Vijiji 46 vilivyoruhusiwa ni vile vilinavyoendesha shughuli za kibinadamu kwenye eneo kinga la mita 500 linalotenganisha vijiji hivyo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Maswa pamoja na Pori la akiba la Kijereshi.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na uamuzi huo wa serikali uliotolewa mkoa utakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka zote zilizopo ndani ya mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu, Gabriel Zakaria akichangia hoja wakati wa kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta na uongozi wa mkoa wa Simiyu tarehe 17 Oktoba 2022.
"Kamati ya wataalamu inayojumuisha wataalamu kutoka ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na taasisi zetu za uhifadhi ilianza kazi za tathmini katika vijiji husika mwezi septemba 2022,"amesema Dkt.Mabula.
Dkt.Mabula ameongeza kuwa, tathmini iliyofanyika inahusisha kufanya vikao na viongozi wa serikali za vijiji na kuembelea eneo la kinga la mita mia tano kubaini matumizi yaliyopo sasa.
Baadhi ya Mapendekezo ya kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni pamoja na kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi sambamba na kuhakiki na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.