NA HAPPINESS SHAYO-WMU
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaasa wananchi wa Kitongoji cha Nkanka ,Kijiji cha Itumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, kuheshimu maeneo yatakayobaki baada ya kumegewa sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range baada ya mipaka kuwekwa.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjJAx7USo-r3AuPRHYgpID9qJibbQZkd_tXzXAgGrA3kgsGR83OVP4_7kXMRrhUG_B7jQT_i1pbSP2GfvebQn_IpF8oRCIzli2z_AYgWwEVa5qv2PhInD41SAmiw31TC7rGjcGLEWCHPP3ijlNwnxRK2jpdSqxbyE8R9nFFSgawBQBR2qM-Xxj3hm-eNA/s16000/IMG-20221024-WA0015.jpg)
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia Kitongoji cha Nkanka kumegewa sehemu ya hifadhi na kuwataka wananchi kuacha kuendelea kuvamia eneo la msitu huo kwa ajili ya matumizi yao binafsi.
“Sasa niwaombe huruma ya Mheshimiwa Rais isije ikawafanya mkajisahau, ninyi sasa hivi mtakuwa sehemu ya hifadhi mtasimamia na kuhakikisha miti haichomwi, haikatwi hovyo na shughuli za kibinadamu haziingii kwenye eneo hili la hifadhi” amesisitiza.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiE01_2MtjTZEpB-3ZI7ikhNUaboa0dP9LYnUUSBtNuT8fSeyeSYOvQqHURBVboTH1zyfgkutjDHGyNWottIimLXQqb4luyrDKidWxROYqR6EUg9SQp2Fjtsp3hKvxQvYnACv30f8DZDwd0daSwK_VVIlx-EhgHlZvVbwUjiKDLCi6vZFKzqTkdG8CH0Q/s16000/IMG-20221024-WA0013.jpg)
Amefafanua kuwa baada ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na wananchi wa Nkanka, kufanya marudio ya kutambua na kuweka vigingi wananchi hawataruhusiwa kuingia tena ndani ya hifadhi hiyo.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjVoxuZ1HBBEyvKwy-RxJRaTBx4gbIiu_9BfGnW5vwIOaP1SeaAhKplYLJ3G_e4Eyx1rzwflt9hypa8REf6kTI0cxWPb_fJqAHUZcYiL9KeRJVnxI3aktqoA9t2hQ26m5daraSicsTdhBL0A93UVjePwq6HGykxAyFIuKkM-T9O8BUapMeNxH0m4yFXqA/s16000/IMG-20221024-WA0014.jpg)
Awali akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Masanja amewaomba kuendelea kutatua migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu mengine ya kitaifa.