TAMISEMI Queens yaendeleza ubabe Ligi Kuu ya Netiboli

NA PETER STEPHEN

MABINGWA watetezi wa Kombe la Ligi Kuu ya Netiboli Tanzania, TAMISEMI Queens imeendeleza wimbi lake la ushindi baada jana kuichapa bila huruma timu ya Mafunzo kutoka Zanzibar, katika michuano inayoendelea katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mchezaji wa kati wa Mafunzo Zuwena Nassor akijiandaa kurusha mpira kuelekea goli la Tamisemi huku akizongwa na mchezaji Mecklina Lucas (aliyeruka juu) wa Tamisemi Queens katika mchezo uliomalizika kwa Tamisemi kuifunga Mafunzo magoli 40-35.

TAMISEMI Queens ikijivunia mastaa wake watano wanaochezea timu ya Taifa ya netiboli walianza mchezo huo kwa kasi ya aina yake, na kuwalazimu wachezaji wa Mafunzo kuikabili vilivyo kasi ya Tamisemi iliyokuwa ikiongozwa na mfungaji wao hatari, Lilian Jovin.

Kutokana na kasi ya mchezo huo, waamuzi walilazimika kupuliza filimbi mara kwa mara kutokana na faulo walizokuwa wakichezeana wachezaji wa pande zote mbili.

Hadi robo ya tatu ya mchezo huo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini walikuwa ni Mastaa wa Tamisemi Queens waliobadili mwelekeo wa mchezo huo katika robo ya mwisho kufuatia uimara wa beki wake mahiri (GD) Mersiana Samwel ambaye alikuwa akizuia hatari zote kutoka kwa wachezaji Adela Miraji (GS) na Mainda Rodgers (GA) wa Mafunzo ambao walikuwa wakilisakama goli la Tamisemi kama nyuki.

Huu ni mchezo wanne kwa TAMISEMI Queens kushinda mechi zake mfululizo, na hivyo kuendelea kujisafishia njia ya kulitetea vema kombe lake la Ligi kuu ya Netiboli Tanzania.
Mchezaji wa pembeni wa timu ya Mafunzo ya Zanzibar Jane Josephat ‘aliye na mpira’ akitafuta mbinu ya kuwatoka wachezaji wa TAMISEMI Queens Mersiana Samwel (GD) kushoto aliyevaa jezi nyeusi na Sophia Komba (WA) wakati wa mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika jana katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambapo Tamisemi ilishinda mchezo huo magoli 40-35.

Mara baada ya mchezo kumalizika wachezaji wa TAMISEMI Queens walishangilia ushindi huo kwa staili ya aina yake baada ya kujikusanya kwa pamoja na kukata keki maalum iliyoletwa uwanjani hapo kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya kocha wao Maimuna Rajabu Kitete.

Akizungumza uwanjani hapo Kocha Maimuna aliwasifu wachezaji wake kwa namna walivyojituma uwanjani na kuhakikisha timu yake inapata ushindi huo na pia kupongeza uwezo wa wachezaji wa timu pinzani kwa jinsi wanavyoleta ushindani dhidi ya timu yake.

“Mashindano ya mwaka huu yana ushindani wa aina yake kwani kila timu tunayokutana nayo inaleta upinzani wa hali ya juu, kila timu imejiandaa kuchukua ubingwa,” amesema.

Mbali na mchezo huo, matokeo ya michezo mingine iliyochezwa juzi na jana yanaonyesha timu za Mafunzo na JKU zilitoka sare kwa kufungana magoli 44-44, JKT Mbweni 59-Zimamoto 44, Nyika 59- Chuo Kikuu Kampala 39, KVZ 55- Magereza Tanzania 32.
Mchezaji Adela Miraji (GS) wa Mafunzo akifunga mojawapo ya magoli yake dhidi ya TAMISEMI Queens katika mchezo uliofanyika jana katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambapo Tamisemi ilishinda mchezo huo magoli 40-35.

Kadhalika Zimamoto 38-KVZ 49, JKU 46-Nyika 51, Magereza Tanzania 41-JKT Mbweni 45 na Chuo Kikuu Kampala 49-Warriors 36.

Michezo minne inatarajiwa kupigwa leo katika mwendelezo wa mashindano ya Ligi Kuu ya Netiboli Tanzania ukiwemo mchezo mkali na wa kusisimua kati ya Tamisemi dhidi ya Nyika Queens kutoka mkoa wa Pwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news