'Tanzania imetupa heshima kubwa kuelekea Oktoba 29 pale JICC'

NA GODFREY NNKO

WAWAKILISHI na washiriki mbalimbali wa Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani ambayo yanafanyika hapa nchini Oktoba 29, 2022 wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa maandalizi mazuri na huduma wanazopatiwa.
Wamesema, tangu waingie hapa nchini kwa ajili ya kuendelea na maandalizi kupitia kambi ambayo imewekwa jijini Dar es Salaam wanafarijika kuona Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwapatia ushirikiano wa hali ya juu.

Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti Oktoba 24, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara waliyofanya katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JICC), Daraja la Tanzanite na ufukwe wa Coco Beach kwa ajili ya kujionea hatua za maandalizi na mandhari ya jiji.

"Nimejifunza kuwa, Watanzania ni watu wakarimu mno. Hakika tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi na huduma nzuri ambazo tunapatiwa tangu tufike hapa kambini,"amesema mmoja wa wawakilishi wa mashindano hayo kutoka India.
Aidha,maafisa kutoka baadhi ya Serikali waliowasindikiza washiriki hao baada ya kushuhudia uwekezaji uliofanywa katika Daraja la Tanzanite wamesema, uwekezaji wa miundombinu unaofanywa na Tanzania unapaswa kupongezwa kwa kuwa,unanuia kupaisha uchumi nchini.

Kwa upande wake mwakilishi wa Jamhuri ya Zimbabwe kupitia mashindano hayo, Bi.Primrose Madhiba amesema,licha ya undugu wa kaka na dada uliopo kati ya Tanzania na Zimbabwe, wanajivunia kuona Watanzania na viongozi wa Serikali wamekuwa ni watu wenye upendo, mshikamano na wasikivu.

Awali, Primrose akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa, anaamini atafanya vema katika mashindano hayo kwani, licha ya kujifunza mengi katika kambi pia anapata ushirikiano wa kutosha kutoka serikalini.
"Na pengine undugu wetu ni zaidi ya kaka na dada, lakini tunafarijika sana kwa namna ambavyo tunapewa heshima, hii ni faraja sana, tunashukuru,"amesema Madhiba.

Nasra Swalehe na John Mushi ni wakufunzi wanaofundisha miondoko kwa washiriki wa Tanzania katika kambi inayojiandaa na mashindano hayo wamesema kuwa,washiriki wote wako vizuri kwani wana ari ya kushiriki na kuiletea heshima kubwa Tanzania.
Pia wamesema,maandalizi ni mazuri, kwani washiriki wote sita ambao wanaiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya Dunia wameonesha utayari wa kufanya vema Oktoba 29, 2022.

Aidha, wakufunzi hao wamewahimiza vijana wa Tanzania wanapopata nafasi ya kuliwakilisha Taifa popote kujitoa kwa moyo, ari na bidii ili kupata ushindi kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Naye Rais wa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Afrika (MMDAF),Habibu Mrope amesema kuwa,maandalizi ya mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika Jumamosi ya wiki hii jijini Dar es Salaam yanaendelea vizuri.

Pia amesema, washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania wameendelea kujiandaa katika kambi yao huku kila mmoja akionekana kuwa na ari ya kufanya vema kwa ajili ya kuipeperusha bendera ya Taifa lake na hata kuibuka kidedea.
Awali Rais wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Kimataifa linalojihusisha na Uandaaji wa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Duniani (Miss & Mister Deaf International, Inc), Bi.Bonita Ann Leek amesema, mwaka huu wameamua kuiteua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kidunia kutokana na ukarimu wa Watanzania, upendo, mshikamano na amani iliyopo nchini.

MMDI ni shirika lisilo la faida ambalo limenuia kuwezesha, kuimarisha, na kuunga mkono vipaji vya wanawake na wanaume viziwi ili viweze kutambuliwa na kuendelezwa duniani kwa ustawi bora wa maisha yao na Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Dkt.Emmanuel Ishengoma amesema, Tanzania kama nchi mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya utanashati, urembo na mitindo duniani inatoa ushirikiano wote kwa washiriki ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu mashindano hayo Oktoba 29, 2022.

Mmoja wa maafisa kutoka Serikali ya Zimbabwe ameieleza DIRAMAKINI kuwa, wanatamani kufanya vema zaidi katika mashindano hayo ili mwakani Mungu akijalia waweze kuwa wenyeji.

"Tunatamani haya mashindano kuwa mwenyeji mwakani kwa sababu, tukiyatumia vema kimkakati tutaweza kutangaza fursa zilizopo nchini ikiwemo utalii na uwekezaji. Zimbabwe ina vivutio ingawa si kwa wingi kivile, lakini tunaamini tukivitumia na kuvitangaza vema tutaweza kupiga hatua. Mfano kuanzia kule Mutare, Ziwa Kariba,Hifadhi ya Matobo,Gweru, Great Zimbabwe, Victoria Falls na kwingineko,"amesema afisa huyo katika mazungumzo na DIRAMAKINI.
Kwa sasa, zimesalia siku tatu kabla ya mashindano hayo kufanyika Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JICC) jijini Dar es Salaam ambapo wageni na washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo nchini tayari na wengine wanaendelea kuja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news