NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya maji na usafi wa mazingira nchini ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama. Mhe.Waziri Dkt.Tax akiangalia bwawa lililochimbwa kitaalamu bila kuharibu mazingira na viumbe hai alipotembelea Kituo cha Maji kilichopo chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Poland.
Mhe. Dkt.Tax akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Wojciech Sas alipofika kukitembelea kituo hicho na kujionea maabara mbalimbali za maji.
Hayo yamesemwa Oktoba 17, 2022 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt.Stergomena Tax alipotembelea Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi nchini humo.
Mhe. Dkt.Tax ambaye alikutana na Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na wamiliki wa kampuni mbalimbali za Poland zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maji nchini, amesema, sekta ya maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele nchini, kwani zinagusa maisha ya wananchi wote wa mijini na vijijini na kwamba wanahitajika wawekezaji makini na wenye tija kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuiboresha.
Amesema, miji mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam inaendelea kukua kwa kasi hivyo upo umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama lakini pia kuendelea kutunza mazingira.
“Maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali ili kuhakikisha sekta hii inaboreshwa zaidi hususan kwenye teknolojia ya kisasa ya usimamizi wa maji ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu,”amesema Dkt.Tax.
Mhe.Waziri Dkt.Tax akizungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw cha nchini Poland kuhusu masuala ya ushirikiano katika sekta za elimu na maji. Kushoto kwake ni Prof. Zasada, Mkuu wa Chuo hicho akifuatiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Marta Mendel na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Mhe. Krystof Buzalski. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland, Mhe.Balozi Abdallah Possi.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Zasada akizungumza kumkaribisha Mhe. Dkt Tax alipotembelea Chuoni hapo.
Pia amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazosimamia sekta ya maji nchini ikiwemo Wizara ya Maji ili kwa pamoja kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri chuoni hapo, Mkuu wa Chuo, Prof. Michal Zasada amesema chuo hicho ambacho kimejikita katika ufundishaji wa teknolojia mpya ya usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, kipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sekta hiyo kutoka nchini.
“Tumefarijika kutembelewa na wewe Mhe.Waziri na ujumbe wako kutoka Tanzania. chuo chetu kinatoa kozi mbalimbali za Shahada na Shahada ya Uzamili katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya maji. Tayari wataalam kadhaa kutoka sekta ya maji wamewahi kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo hapa chuoni. Tunaendelea kuwakaribisha Watanzania kujiunga na program mbalimbali za mafunzo hususan za sekta ya maji zinazotolewa chuoni hapa,”amesema Prof.Zasada.
Wakati wa Mkutano huo Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na sekta ya maji na usafi wa mazingira za Poland ikiwemo ile ya Asseco ziliwasilisha mada na kueleza utayari wao wa kuwekeza katika sekta ya maji kwa kuanza na miji ya Dodoma na Dar es Salaam.
Akiwa chuoni hapo Mhe. Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea maabara za kisasa za usimamizi wa maji pamoja na kujionea mradi wa maji unaotumia teknolojia ya kisasa unaotekelezwa na chuo hicho.
Mhe. Dkt.Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.