NA MWANDISHI WETU
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeungana na nchini nyingine Afrika katika kushiriki mkutano wa Africa Oil Week unaofanyika katika Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini kwa siku 5 mfululizo kuanzia tarehe 3 hadi 7 Oktoba 2022.
Mkutano huu unaowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi unalenga kujadili kuhusu mabadiliko ya matumizi ya nishati kutoka nishati zenye kutoa hewa ukaa nyingi kuelekea nishati zenye kutoa kiasi kidogo cha hewa ukaa ikiwa ni mikakati ya kidunia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Washiriki mbalimbali wa Mkutano wa Africa Oil Week wakipata taarifa mbalimbali za fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi Tanzania katika banda la maonesho la TPDC.
Katika Mkutano huo Tanzania imewakilishwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato (Mb) ambae pia ameambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue pamoja na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TPDC na PURA.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato akizungumza katika Mkutano Africa Oil Week sambamba na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka Uganda, Mhe. Ruth Nankabirwa na Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Libya, Mhe. Mohamed Mahemed Oun.
Akiongea katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato alisema Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuchochea matumizi ya gesi asilia ambayo ni nishati safi na salama kwa mazingira ambapo kwa sasa asilimia zaidi ya 60 ya umeme katika gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia ambayo imekuwa ni mbadala wa mafuta mazito.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya TPDC iliyoshiriki Mkutano wa Africa Oil Week unaofanyika Jijini Cape Town, Afrika Kusini. Wengine katika picha kuanzia kulia ni Ndg. Kelvin Komba (Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu TPDC), Ndg. Paul Makanza (Mkurugenzi wa Bodi ya TPDC), Bi. Venosa Ngowi (Meneja Utafutaji TPDC) na Dkt. Wellington Hudson (Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi TPDC).
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue alieleza ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Africa Oil Week unatoa nafasi ya kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya mafuta na gesi na kuendelea kujitangaza kama nchi yenye mazingira rafiki ya uwekezaji.
Tunashiriki mkutano huu tukiwa na malengo ya kimkakati ya kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta yetu ya mafuta na gesi Tanzania na pia kuonyesha maendeleo ambayo tumeyafikia sisi kama nchi katika kuendeleza rasilimali asilia hususan gesi asilia alieleza Balozi Sefue.
Katika kuhakikisha hili linafanikiwa, TPDC kama Shirika la Taifa la Mafuta limeweka banda la maonesho na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
Tags
Biashara
Biashara na Masoko
Biashara na Uwekezaji
Habari
Kimataifa
Kituo cha Uwekezaji Tanzania
TPDC