NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya inayohusika na kitengo cha makasha katika Bandari ya Dar es Salaam,(TICTS) imewasilisha serikalini mpango madhubuti wa kuwekeza shilingi trilioni 1.15 kwenye mifumo ya upakiaji na upakuaji makasha bandarini hapo.
Winchi aina ya RTG mali ya kampuni ya TICTS ikipanga makasha kwenye eneo hilo la Bandari ya Dar es Salaam.
Kampuni hiyo imesema hayo kupitia taarifa yake kwa umma ambapo pia imesema imefurahishwa na kuboreka kwa uhusiano wake na shirika hodhi la bandari yaani Mamlaka ya Bandari Tanzania, hatua ambayo imefanikisha kushamiri kwa utendaji wake kwa mwaka uliopita.
Taarifa hiyo imesema mwaka 2021, muda wa meli kusubiria kuingia bandarini ulikuwa ni mkubwa, hivyo kusababisha mlundikano wa meli kwenye bahari kuu.
Hata hivyo kampuni yetu kupitia kwa kampuni mama ya Hutchison Ports ya China,ilifanikiwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 12.5 katika vifaa na mifumo na hivyo kuongeza ufanisi na kulitatua na kulimaliza kabisa tatizo hilo na sasa hali ni shwari,taarifa hiyo imeongeza.
Kutokana na uwekezaji huo mpya TICTS imeweza kuongeza idadi ya makasha yanayopitia kwenye kitengo hicho kutoka 50,000 kwenye mwezi wenye mizigo mingi na sasa inakaribia makasha 70,000, na kwamba sasa hali inakoelekea ni kushughulikia makasha zaidi ya 700,000 kwa mwaka mmoja.
"TICTS tunaamini kuwa hii ni habari njema kwa wafanyabiashara wa kimataifa nchini Tanzania na majirani zake wanaotegemea Dar es Salaam kama mlango wao mkuu wa biashara pamoja na bandari kama chaguo lao,"imeeleza.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo ya mwaka 2022,kumekuwepo na changamoto kadhaa ikiwemo vifaa vya kazi kuharibiwa katika mazingira ya kutatanisha,mambo ambayo yalipekekea wao kuvirekebisha vifaa hivyo kwa gharama kubwa pamoja na kutoa ripoti polisi kwa waharibifu hao.
"Wakati wote huo kampuni yetu pia imefanya kazi kwa karibu sana na mamlaka ya bandari na hilo limesaidia sana kupata msaada wa kiufundi na ushauri, pale tunapouhitaji kutoka kwa mamlaka hiyo ambayo ni mmiliki wa eneo zima la bandari,"imesema.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa TICTS, Bw. Matthew Clifft amesema, “TICTS inazishukuru Mamlaka ya Bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ushirikiano mzuri kutoka kwa serikali ya Tanzania, lakini pia kutoka wadau mbalimbali wa bandari kwa ushirikiano wao pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kufanya kazi kwa makini,"amesema.
Amesema, katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana mwaka huu,TICTS inakusudia kufanya vizuri zaidi ili kuendeleza eneo hili la bandari.
Winchi aina ya SGG mali ya kampuni ya makasha ya TICTS ikipakia makasha kwenye meli eneo linaloendeshwa na kampuni hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam.
"Gati nambari 8 hadi 11 zimefikia wakati wa kufanyiwa ukarabati na kwa sababu hiyo kampuni mama yetu imeahidi kufanikisha jambo hilo ili kuhakikisha eneo hili la bandari liendelee kuwa na vifango bora vya ufanisi katika kuhudumia mizigo ya makasha,"amesema.
Amesema, kampuni hiyo ambayo imekuwepo hapa nchini kwa miaka 20 sasa imesema sambamba na mkakati wa serikali wa kuchagiza uwekezaji kutoka nje ya nchi na kukuza uchumi,mipango yake ya uwekezaji zaidi katika eneo hilo siyo tu itaongeza ufanisi lakini pia itakuza ajira huku ikiunganisha bandari na miundombinu mingine iliyoko nchini ikiwemo vituo vya makasha yaani ICDs pamoja na reli mpya ya umeme inayojengwa.
TICTS ni kampuni tanzu ya Hutchison Ports Hongkong nchini China ikiwa na inaendesha bandari 52 katika nchi 26 Barani Asia, Mashariki ya Kati, Afrika,Ulaya,Amerika Kusini na Australia.