NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imesema itaendelea kuchukua tahadhari zote kupitia mifumo yake ya udhibiti, ili kubaini endapo dawa inayosadikiwa kusababisha vifo vya watoto 66 nchini Gambia zitafika nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Adam Fimbo leo katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, amesema dawa hizo hazijawahi kusajiliwa nchini.
Dawa hizo za Promethazine oral solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Syrup na Margrip N Cold Syrup zinatengenezwa na kiwanda chenye jina la Maiden Pharmceutical Limited, iliyopo India zilipimwa na kukutwa na viambata vya sumu.
Fimbo amesema dawa hizo zimeonekana kuwa na viambata vinavyosababisha madhara ya kiafya, ikiwa ni pamoja na vifo kwa watumiaji hasa watoto.
“Dawa hizo zimepimwa na kukutwa na viambata vinavyojulikana kama diethlene glycol na ethylene glycol, ambavyo husababisha madhara na hata vifo kwa watumiaji.
“TMDA inapenda kuutarifu umma kuwa dawa hizo zote hazipo katika soko la nchi yetu na hazijawahi kusajiliwa, ili kutumika hapa nchini,” amesema.