TOBA YA KUJINASIBU

NA ADELADIUS MAKWEGA

OKTOBA 22, 2022 nikiwa Mbagala jijini Dar es Salaam nilipata wasaa wa kusali Mtaa wa Mtakatifu Stephano-Sabasaba, jumuiya ya Yohane Mbatizaji, Parokia ya Mbagala-Kizuiani, Kanisa la Kutukuka kwa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Mwanakwetu nikiwa katika jumuiya hiyo idadi ya waamini waliofika kusali ilikaribia 20 na tukasali vizuri huku na mimi nikiwa mgeni mwenyeji.

Mgeni mwenyeji mimi katika jumuiya hii ilikuwa kwa sababu tangu jumuiya hii inatafutiwa jina mimi nilikuwa kijana mwenye umri wa kujitambua miaka hiyo ya 1990.

Siku hii nilibahatisha kuwaona watu wawili ambao walikuwapo wakati huo sasa ni wazee kabisa; Mwalimu Mng’ande na Mzee Marando. Wakati huo walikuwa vijana kabisa na wakiwa watumishi wa Serikali.

Mzee Marando akiwa mtumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania naye Mwalimu Mng’ande alikuwa mwalimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke akisomesha Shule ya Msingi Sokoine. 
Wazee wangu hawa wakati huo nywele zao zilikuwa nyeusi, lakini sasa vichwa vyao vimejaa mvi, taswira hiyo ya nywele nyeupe za wazee hao ilinipa picha miaka iinavyosonga.

Majibu ya miaka kusonga yalithibishwa na macho yangu kushindwa kuyaona maandishi ya somo la injili kutoka kwa Luka18, 9-14. Wazee wangu hawa wawili wanatamani nywele zao ziwe nyeusi, lakini muda umepita naye mwanakwetu anatamani macho yake yaone bila miwani lakini yanashindwa,

Injili hii ilisomwa;

“Watu wawili walikwenda hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. yule Farisayo alisimama akasali kimoyomoyo. ‘Ninakushukuru Mungu kwa sababu mimi si kama watu wengine: wany ang’anyi, wadhalimu, wazinzi, au kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma na kutoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.'Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali. Hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni; bali alijipiga kifuani kwa majuto akasema, ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’ Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu na wala si yule Farisayo. Kwa maana ye yote ajikwezaye atashushwa na ye yote ajinyenyekezaye, atainuliwa.”

Kumbuka tupo tunasali jumuiya, mwongozaji wa sala hii aliomba angalau wana jumuiya hii watafakari injili hii kwa kusema neno walilolielewa katika mfano huu.

Tafakari kadhaa zilitolewa huku toba ya mtoza ushuru ilivyokuwa njema ikinadiwa mno na toba ya Farisayo ilivyokosa unyenyekevu ikitia simanzi kwangu mimi. Jumuiya ilipomaliza kusali kila mmoja akurudi kwake, kwa kuwa jumuiya hii ilisali kwetu binafsi nilibaki katika kiti nikilitafakari sana somo hilo.

“Je toba nzuri ya mtoza ushuru inaweza kutumika kuhalalisha maovu yake aliyokuwa akiyafanya katika kutoza ushuru, iwe kupora mali za watu wakati akitimiza majukumu hayo?Je inaharamisha mema ya Farisayo yaliyotajwa katika mfano huu? Mathalani kwa kutokuwa mzinzi, kutokuwa mpokonyaji wa mali za watu, kutoa zaka na kufunga ?”

Kwa hakika mfano huu niliona unajenga dhana njema ya kusisitiza namna njema ya kuomba toba mbele ya Mungu, lakini ikiyapa kisogo matendo mema. Nadhani dhana ya kutubu, yule anayefanya hivyo anaanza upya kabisa, anakuwa hana dhambi. Kulinda usafi huo nadhani ni lazima awe na matendo mema ambayo farisayo aliyataja kuwa aliyatenda, naye mtoza ushuru akipungukiwa nayo.

Binafsi ninaamini kuwa mfano huu unatumiwa sana kujenga dhana ya toba ya unyenyekevu, huku wasomaji wengi wakijificha kwa mtoza ushuru na unyenyekevu wake na kumkataa Farisayo na toba yake ya kujinasibu. Binafsi ninaamini kuwa sote tunapaswa kuwapenda farisayo na mtoza ushuru maana wao walitumika tu kama ishara kwetu ili tujifunze matendo mema na toba ya unyenyekevu.

Binafsi ninaamini hatupaswi kuchukua moja na kuacha mengine. Mwanakwetu upo? Naomba kwa leo niishie hapo.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news